UCHAGUZI MAREKANI 2020

Uamuzi wa nani kuwa rais wa Marekani, wabaki katika majimbo muhimu

Kura zinaendelea kuhesabiwa nchini Marekani
Kura zinaendelea kuhesabiwa nchini Marekani AFP

Matokeo ya uchaguzi mkuu wa Marekani, yanaonesha wagombea wote wawili wanafukuzana kwa karibu, wakati huu kura za maoni zikionesha rais Donald Trump, akifanya vizuri katika majimbo aliyotarajiwa kushinda.

Matangazo ya kibiashara

Hadi sasa matokeo yanaonesha Donald Trump na mpinzania wake Joe Biden, hawapishani sana katika majimbo yaliyotarajiwa kuwa na ushindani mkali.

Rais Trump tayari anaonekana kushinda jimbo la Florida, jimbo ambalo linamuongezea nguvu kuelekea kupata ushindi ikiwa atafanya vizuri katika majimbo mengine.

Hata hivyo Joe Bidenm kwa upande wake amefanikiwa kuchomoza na ushindi katika jimbo la Arizona.

Majimbo mengine yanayotarajiwa kuwa na ushindani ni pamoja na yale ya Georgia, Pennsylvania ambako Trump anaongoza, Wisconsin, Michigan na North Carolina.

Wakati huu kukiwa na ushindani mkali katika majimbo muhimu, hata hivyo raia watalazimika kusubiri kwa siku kadhaa kujua matokeo rasmi, kwakuwa baadhi ya majimbo yatalazimika kuendelea kuhesabu kura hata baada ya vituo kufungwa.

Zaidi ya watu milioni 100 tayari wameshapiga kura nchini Marekani, katika moja ya uchaguzi ambao unatajwa kuwa utashuhudia idadi kubwa zaidi ya wapiga kura wakijitokeza.