MAREKANI-UCHAGUZI-SIASA-USALAMA

Biden kuelekea kupata ushindi, Trump afungua kesi mahakamani

Kituo cha kupigia kura huko Bloomington, Indiana Juni 2, 2020, siku ya uchaguzi wa mapema.
Kituo cha kupigia kura huko Bloomington, Indiana Juni 2, 2020, siku ya uchaguzi wa mapema. Jeremy Hogan/SOPA Images/LightRocket via Getty Images

Mgombea wa chama Democratic kwenye uchaguzi wa urais nchini Marekani Joe Biden, anaelekea kupata ushindi licha ya ushindani mkali kutoka kwa mpinzani wake rais Donald Trump.

Matangazo ya kibiashara

Vyombo vya Habari nchini Marekani, vinaripoti kuwa Biden ameshinda majimbo ya Wisconsin na Michigan na kumweka katika nafasi nzuri ya kushinda na sasa anahitaji tu kura sita ili kupata kura 270 za wajumbe ili kutanagzwa mshindi.

Matumaini ya Joe Biden ya kuingia Ikulu yalizidi kuwa makubwa baada ya kulichukua jimbo la Michigan lenye kura 16 za wajumbe maalumu. Joe Biden pia ameshinda kwenye jimbo lingine muhimu la Wisconsin.

Biden amesema ana uhakika wa kupata ushindi.

Wakati huo huo Rais Donald Trump amefungua kesi ya kupinga uhesabuji wa kura katika majimbo muhimu yanayosalia ya Wisconsin, Georgia, Pennsylvania na Michigan.

Trump amedai kuwa alikuwa anaelekea kupata ushindi lakini kuna njama za udanganyifu zinazofanyika na upande wa chama cha Democratic ili ashindwe.

Waendesha kampeni wa kambi ya Trump wamewalaumu maafisa wa uchaguzi kwa kuwazuia mawakala wao kuzikaribia sehemu za kuhesabia kura kwenye jimbo la Pennsylvania. Mpaka sasa Trump amepata kura 214 za wajumbe wa baraza maalumu.