MAREKANI-UCHAGUZI-SIASA-USALAMA

Marekani 2020: Trump aapa kuendelea na mapambano yake mahakamani dhidi ya matokeo ya uchaguzi

Donald Trump ameahidi kuendelea na mapambano yake dhidi ya kile alichokiita matokeo ya uchaguzi yaliyogubikwa udanganyifu mkubwa, wakati mpinzani wake wa Joe Biden anaonekana kushinda uchaguzi.

Rais wa Marekani Donald Trump.
Rais wa Marekani Donald Trump. REUTERS/Kevin Lamarque
Matangazo ya kibiashara

Joe Biden amezungumza na umma wa Wamarekani na kutaja tena vipaumbele vyake katika kipindi hiki akiashiria ushindi wa urais.

Joe Biden anaongoza kwa kura ambazo zimehesabiwa katika majimbo yenye ushindani mkali ya Georgia na Pennsylvania; Hata hivyo zoezi la uheshabuji wa kura linaendelea.

Joe Biden aliye na umri wa miaka 77 na ambaye pia ni makamu wa zamani wa rais huenda akawa rais mpya ikiwa atashinda kura katika jimbo la Pennsylvania au kwa kushinda majimbo mawili kati ya Georgia, Nevada na Arizona.

"Tutaendelea na mchakato huu kwa njia zote zinazoruhusiwa kisheria ili kuhakikisha kuwa wananchi wa Marekani wana imani na serikali yetu. Kamwe sitaacha kuwatetea na kutetea taifa letu," rais anayemaliza muda wake amesema katika taarifa.

Rufaa kadhaa tayari zimewasilishwa katika majimbo kadhaa na rais Trump anaendelea kushtumu kwamba uchaguzi huo uligubikwa na udanganyifu mkubwa bila kutoa uthibitisho.

Kulingana na vyanzo viwili vilivyo karibu na mpango huo, Kamati ya Kitaifa ya Chama cha Republican inatarajia kukusanya dola milioni 60 kufadhili kesi za kisheria zinazopinga matokeo.