MAREKANI-ISRAEL-UCHAGUZI-SIASA

Uchaguzi Marekani: Benjamin Netanyahu ampongeza Joe Biden kwa ushindi wake

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu. Sebastian Scheiner/Pool via REUTERS

Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu amekaribisha ushindi wa mgombea urais wa chama cha Democratic Joe Biden katika uchaguzi wa urais uliofanyika Novemba 3.

Matangazo ya kibiashara

Benjamin Netanyahu amemwita Joe Biden "rafiki mkubwa wa Israeli". “Hongera sana Joe Biden na Kamala Harris. Joe, tumefahamiana kwa karibu miaka 40, uhusiano wetu ni mzuri, na najua wewe ni rafiki mzuri wa Israeli. Natumai, kwa ushirikiano wa nyinyi wote wawili, uhusiano wa nchi hizi mbili, Marekani na Israeli utaendelea kuimarika, ”aliandika Benjamin Netanyahu kwenye ukurasa wake ya Twitter.

Wakati huo wademocrats wanaendelea kusherehekea ushindi wa Joe Biden, ambaye alijitangaza mwenyewe kuwa rais wa 46 wa Marekani Jumamosi usiku na kuahidi katika hotuba yake ya kwanza kwa taifa kama rais mteule kutafuta kuunganisha nchi iliyopoteza maadili yake baada ya miaka minne utawala wa Trump.

Kote nchini, wafuasi wa chama cha Democratic wameendelea kusherehekea ushindi wao katika mchakato wa uchaguzi wa urais uliyodumu wiki moja.

Kuwaunganisha raia na "kuponya majeraha", alisema Joe Biden siku ya Jumamosi, huku akiwashukuru wapiga kura wa Markani kwa kumpa "ushindi wa kishindo" na amehidi kuwa atakuwa "rais aatakayewaunganisha wananchi na sio aatakayegawanya".

Kama mgombea mwenza Kamala Harris aliyemtangulia kwenye huko Chase Center katika mji wa Wilmington, mbele ya umati wa wafuasi wake, Joe Biden alisema ni "wakati wa kuponya Marekani", "kuponya majeraha" . "Wacha tuone, tuzungumze", "wacha tujipe nafasi", aliomba, akiwataka Wamarekani wasiwachukulie tena "wapinzani wao kama maadui".

"Nilifanya kampeni ya kutuliza nyoyo za Wamarekani, kujenga tena uti wa mgongo wa taifa hili, na kuifanya Marekani iheshimiwe tena ulimwenguni," amesema rais mteule.

Mgombea wa chama cha Democratic Joe Biden alishinda uchaguzi wa urais wa Marekani, baada ya kushinda jimbo muhimu la Pennsylvania kwa kupata wajumbe maalumu 20. Kulingana na vyombo vya habari, alizidisha idadi ya 270 inayohitajika kutangazwa mshindi, na kupata kati ya 273 na 284, dhidi ya 214 aliopata Donald Trump.

Hata hivyo zoezi la uhesabuji wa kura linaendelea, kwani majimbo ya Georgia, Arizona, Nevada na North Carolina bado hayajatangaza matokeo yao ya mwisho. Georgia ilitangaza kuwa itarejea kuhesabu upya kura zake.