MAREKANI-TRUMP-CORONA-AFYA

Kwa mara ya kwanza tangu kushindwa kwake, Trump azungumzia juu ya mgogoro wa Covid-19

Rais wa Marekani Donald Trump akizungumza kwa mara ya kwanza tangu mpizani wake Joe Biden atangazwe mshindi wa uchaguzi wa urais.
Rais wa Marekani Donald Trump akizungumza kwa mara ya kwanza tangu mpizani wake Joe Biden atangazwe mshindi wa uchaguzi wa urais. MANDEL NGAN / AFP

Ni kwa mara ya kwanza Donald Trump kuzungumza hadharani tangu Joe Biden atangazwe mshindi wa uchaguzi wa urais wa Novemba 3, 2020.

Matangazo ya kibiashara

Rais hakujibu maswali ya waandishi wa habari, wala hakuzungumzia kuhusu uchaguzi, wala kukiri kushindwa katika uchaguzi huo. Rais Trump amezungumzia tu kuhusu janga la Corona ambalo kwa sasa linavunja rekodi nchini Marekani.

 

Mbele ya waandishi wa habari kwenye bustani ya White House, Donald Trump amekaribisha jinsi utawala wake ulivyosimamia mgogoro wa COVID-19.

Wakati huo huo ameahidi kwamba hivi karibuni atasambaza chanjo iliyotengenezwa na kampuni ya Pfitzer, ambayo bado iko katika hatua ya majaribio.

"Kama ungekuwa utawala tofauti na wangu, kile tulichokifanya kingechukua miaka mitatu, minne au mitano", amejivunia Donald Trump juu ya kupitishwa kwa chanjo ambayo inaendelea kutengenezwa, kabla ya kuongeza "hakuna anayeweza kuamini".

"Jumatatu wiki hii kampuni ya Pfizer ilitangaza kwamba chanjo yake dhidi ya virusi kutoka China ina nguvu zaidi ya 90%. Inazidi matarajio yote, hakuna mtu aliyefikiria kwamba ingefikia kiwango kama hicho. Mnamo mwezi Julai utawala wangu ulifanya makubaliano na kampuni Pfitzer, na ukaipa dola bilioni 1.9 kusaidia kutengenezwa kwa wingi kwa chanjo hiyo na kusambaza dozi milioni mia moja", amebaini Donald Trump.

Mbali na kukiri kushindwa kwake katika uchaguzi wa urais wa hivi karibuni, ameendelea kujijengea imani kuwa ataendelea kusalia kwenye kiti cha urais kwa muhula mwingine, na kubaini kwamba katika katika siku za usoni utawala wake utasambaza chanjo hiyo kwa raia wa nchi hiyo.

"Kwa kweli hatutochukuwa hatua ya kupiga marufuku watu kutotembea, sitafanya hivyo. Utawala huu hautalazimisha hatua hii. hata kutokee nini, ni nani anayejua utawala utakao kuwepo, naamini ukweli utadhihirika siku zijazo," rais Trump amesema.

Kufikia sasa Joe Biden ana kura 306 za wajumbe maalumu dhidi ya 232 ambazo amepata Donald Trump, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Marekani.