MAREKANI-CORONA-AFYA

Donald Trump Jr apatikana na virusi vya Corona

Donald Trump na mtoto wake Don Jr katika kampeni ya uchaguzi huko Des Moines, Iowa, Februari 1, 2016.
Donald Trump na mtoto wake Don Jr katika kampeni ya uchaguzi huko Des Moines, Iowa, Februari 1, 2016. REUTERS/Jim Bourg

Donald Trump Jr, mtoto wa kwanza wa rais wa Marekani Donald Trump, amepimwa na kupatikana na virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID-19, msemaji wake amebaini.

Matangazo ya kibiashara

Donald Trump Jr, ambaye alihudhiuria mara kadhaa katika kampeni za uchaguzi wa urais, kama baba yake, amekuwa akipuuzia athari za janga la COVID-19, ambalo hadi sasa limeua zaidi ya watu 254,000 nchini Marekani.

"Don alipatikana na virusi vya Corona mapema wiki hii na yuko karantini nyumbani kwake tangu alipothibitishiwa matokeo ya vipimo," msemaji wake amesema, na kuongeza kuwa hakuwa na dalili kabisa za ugonjwa huo.

Mwanzoni mwa mwezi wa Julai, rafiki yake wa kike, Kimberly Guilfoyle, mtangazaji wa zamani katika kituo cha Fox News, pia alipatikana na ugonjwa wa COVID-19.

Rais Donald Trump mwenyewe alitangaza mwanzoni mwa mwezi Oktoba kwamba alipatikana na ugonjwa huo, kama vile mkewe Melania. Alilazwa hospitalini kwa siku kadhaa katika hospitali ya jeshi ya Walter Reed katika kitongoji cha Washington.

Siku chache baadaye, Mkewe Melania trump alitangaza kwamba mtoto wao Barron pia aliambukizwa virusi vya Corona.

Taarifa ya Donald Jr, 42, kupatikana na virusi vya Corona inakuja saa chache baada ya Andrew Giuliani, mtoto wa Rudy Giuliani, wakili wa rais wa Marekani kutangazwa kuwa aliambukizwa virusi vya Corona.