MAREKANI-DONALD TRUMP

Marekani 2020: Trump kuondoka White House ikiwa ushindi wa Biden utathibitishwa

Rais wa Marekani, Donald Trump.
Rais wa Marekani, Donald Trump. Brendan Smialowski / AFP

Rais wa Marekani Donald Trump amesema kwamba ataondoka Ikulu ikiwa jopo la wajumbe maalumu watathibitisha ushindi wa Joe Biden.  

Matangazo ya kibiashara

Ingawa anaonekana kukubali kushindwa, Donald Trump ameendelea kusema kuwa uchaguzi huo uligubikwa na udanganyifu mkubwa.

 

Hata hivyo madai ya Bw. Trump kuhusu udanganyifu huo hayana uthibitisho hadi sasa.

 

"Uchaguzi huu uligubikwa na wizi wa kura," amebaini Donald Trump, bila hata hivyo kutoa ushahidi wowote kuhusiana na wizi huo.

 

Donald Trump alitoa tangazo hilo wakati wa hotuba ya kijadi kwa wanajeshi wa Marekani wakati wa sherehe ya Thanksgiving.

 

Joe Biden alishinda uchaguzi wa urais wa Novemba 3 baada ya kupata kura 306 za wajumbe maalumu dhidi ya 232 za Donald Trump, na inatarajia kuwa jopo la wajumbe maalumu litakuna Desemba 14.

 

Akijibu ikiwa ataondoka Ikulu iwapo jopo la wajumbe maalumu litampigia kura Joe Biden, Donald Trump amesema, "Kwa kweli nitafanya hivyo. Kwa kweli nitaondoka."

 

"Lakini nadhani mambo yatakuwa mazuri Januari 20," ameongeza.

 

Wawakilishi wa kura za wajumbe watakutana mwezi ujao kuidhinisha rasmi kura zilizopigwa huku Joe Biden wa chama cha Democratic akisubiri kuapishwa kuwa rais Januari 20.