MAREKANI-COVID19

Chanjo ya COVID-19 kuanza kutolewa Marekani

Moja ya chanjo ya Covid 19 ambayo itatumika Marekani.
Moja ya chanjo ya Covid 19 ambayo itatumika Marekani. Reuters

Chanjo ya virusi vya corona iliyotengenezwa na kampuni mbili za Pfizer na BioNTech itaanza kutolewa kwa mara ya kwanza leo Jumatatu Desemba 14, siku kadhaa tangu matumizi yake yalipoidhinishwa, kulingana na maafisa aw Marekani.

Matangazo ya kibiashara

Katika awamu hiyo ya kwanza watu milioni 3 watapatiwa chanjo, huku watumishi wa afya na wahudumu walio mstari wa mbele watapewa kipaumbele katika utoaji wa chanjo dhidi ya virusi vya Corona.

Zoezi la utoaji chanjo litaanza kwa asilimia 100, kwa mujibu wa Jenerali wa Jeshi la Marekani anayesimamia usambazaji wa  chanjo hiyo, Gus Perna, wakati Dozi za kwanza zilisafirishwa jana Jumapili.

“Jumatatu vituo vya kutolea chanjo 145 vitakuwa vimepokea shehena ya kwanza, huku vituo 425 vitapelekewa chanjo siku ya Jumanne na chanjo hiyo itapokelewa pia kwenye vituo vingine 66 siku ya Jumatano, “ amesema Jenerali Gus Perna.

Kampuni ya Pfizer imesema kiasi dozi milioni 25 zinaweza kuwa tayari kwa ajili ya kutimika nchini Marekani ifikapo mwishoni mwa mwezi Disemba. Hivi sasa nchi hiyo imeagiza dozi milioni 100.

Kampuni inayotengeneza chanjo hiyo imesema inafanya kazi na washirika wengine kuanza kusafirisha chanjo kwa kutumia magari ya mizigo kutoka kwenye maghala yake yaliyoko kwenye majimbo Michigan na Wisconsin  kwenda majimbo yote 50 ya Marekani.

Chanjo hiyo ni lazima ihafidhiwe kwenye baridi ya nyuzi -70 C, hali inayoleta changamoto itakayotatuliwa kwa kutumia barafu na kontena maalum zilizotengenezwa kwa ajili ya kuhifadhi shehena yake.