MAREKANI-COVID19

Marekani 2020: Maseneta wa chama cha Republican watambua ushindi wa Joe Biden

Kiongozi wa wengi katika bunge la seneti Marekani, Mitch McConnell.
Kiongozi wa wengi katika bunge la seneti Marekani, Mitch McConnell. 路透社

Maseneta kadhaa wa chama cha Republican nchini Marekani wamemtambua mgombea wa chama cha Democratic Joe Biden kama rais mteule wa nchi hiyo baada ya Jopo la wajumbe maalumu lenye nguvu ya kumchagua rais wa Marekani, kuthibitisha ushindi wake.

Matangazo ya kibiashara

Kuthibitishwa kwa ushindi huo ni mojawapo ya hatua alizohitaji Bw. Biden ili kumuwezesha kuchukua mamlaka ya urais.

Wakati huo huo wabunge hao wamefutilia mbali wazo la kujaribu kupinga uchaguzi wa urais katika bunge la Congress.

Wakati baadhi ya wabunge ambao wanaendelea kumuunga mkono rais Donald Trump wakijaribu kushawishi wengine kwa kupinga ushindi wa Joe Biden, idadi kubwa ya wabunge wa chama cha Republican inaonekana kuwa tayari kumuangusha Donald Trump na kumtambua Joe Biden kama mshindi, zaidi ya mwezi mmoja baada ya uchaguz wa urais.

Seneta John Thune amesema wabunge wana haki ya kupinga kura za uchaguzi. Lakini pia ameongeza kuwa ni "wakati wa kusonga mbele" na kwamba mara tu Joe Biden "amevuka kizingiti cha kura 270" katika jopo la wajumbe maalumu lenye nguvu ya kumchagua rais wa Marekani, maarufu kama Electoral College, anapaswa moja kwa moja kuwa rais, hakuna hoja zingine, amebaini Seneta John Thune.

Kulingana na jopo hilo Joe Biden alishinda kwa kura 306 dhidi ya 232 alizopata Donald Trump. Matokeo yatatangazwa Januari 6 katika Bunge la Congress, hata kama rais anayemaliza muda wake bado anakataa kutambua ushindi wa mpinzani wake.