MAREKANI-JOE BIDEN

Coronavirus: Biden kupewa chanjo wiki ijayo

Rais mteule wa Marekani, Joe Biden.
Rais mteule wa Marekani, Joe Biden. AP Photo/Matt Slocum

Rais mteule wa Marekani Joe Biden anatarajia kupewa chanjo dhidi ya COVID-19  wiki ijayo, wamesema wajumbe wa timu ya mpito waliopewa jukumu la kuandaa kuwasili kwake kama rais wa nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Makamu wa rais wa Marekani Mike Pence anatarajia kupewa chanjo leo Ijumaa, kulingana na vyanzo kutoka Ikulu ya White House.

Wawili hao watapewa chanjo hadharani ili kuwahakikishia raia na kujenga imani kwa chanjo hiyo.

Rais Donald Trump pia atapewa chanjo mara tu timu yake ya matibabu itakapoona inafaa.

Dozi za kwanza za chanjo imehifadhiwa ili kutumiwa kama kipaumbele kwa wafanyakazi wa afya, watu wanaoishi katika vituo vya matibabu na kijamii, na pia kwa baadhi ya maafisa wa serikali.

Katika awamu ya kwanza, dozi milioni 2.9 zitasambazwa kote nchini Marekani, ambapo janga hilo limeua karibu watu 300,000 katika kipindi cha miezi kumi na moja.

Aidha ikiwa ni wiki moja baada ya kupendekeza idhini ya chanjo ya kwanza dhidi ya COVID-19, kamati ya wataalam nchini Marekani inakutana tena leo Alhamisi kutathmini dawa iliyotengenezwa wakati huu na kampuni ya Marekani ya Moderna, na sindano za kwanza zinatarajiwa kuanzia mwanzoni mwa wiki ijayo.

Mamlaka ya Dawa nchini Marekani inatarajia kutoa idhni ya kutolewa kwa chanjo iliyotengenezwa na kampuni changa ya bioteknolojia muda mfupi baada ya mkutano huu, kwanza mapema Ijumaa kama ilivyofanyika kwa chanjo ya Pfizer / BioNTech.

Marekani, ambayo kwa sasa inakabiliwa na ongezeko kubwa la maambukizi ya COVID-19, basi inaweza kuwa na chanjo mbili mwanzoni mwa juma lijalo, na hivyo kuharakisha kampeni kubwa ya chanjo iliyozinduliwa Jumatatu wiki hii. Marekani ni nchi ya kwanza kuweka sokoni chanjo ya Moderna.

Mkutano wa kamati hii ya ushauri , kama ilivyokuwa wiki moja iliyopita, utarushwa moja kwa moja kwenye wavuti, zoezi la wazi lisilokuwa la kawaida kwa dunia nzima. Karibu wataalam ishirini watalazimika kuthibitisha wakati wa kura kwamba manufaa yanayotolewa kwa kutumia sindano ya chanjo hii yanazidi hatari, kwa watu wazima miaka wenye umri wa miaka 18 na zaidi (miaka 16 kwa chanjo ya Pfizer).