MAREKANI-JOE BIDEN

Marekani: Rais mteule Joe Biden apewa chanjo dhidi ya COVID-19

Rais mteule wa Marekani, Joe Biden, akichoma chanjo ya Covid 19
Rais mteule wa Marekani, Joe Biden, akichoma chanjo ya Covid 19 France24Screenshot

Rais mteule wa Marekani Joe Biden amepokea chanjo ya Pfizer, kuzuia maambukizi ya virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa hatari wa COVID-19.

Matangazo ya kibiashara

Biden amepewa chanjo hiyo na kuonekana moja kwa moja na Wamarekani na anakuwa kiongozi mwingine wa juu baada ya Makamu wa rais Mike Pence na Spika wa Bunge Nancy Pelosi pia kupata chanjo hiyo.

Rais huyo mteule ameeleza sababu ya kupata chanjo hiyo hadharani.

Niko tayari," Joe Biden alisema, akiinua mkono wake. Rais mteule aliongozana na mkewe, ambaye pia alipokea chanjo hiyo, Joe Biden alizungumza kwa muda mrefu na daktari aliyemdunga chanjo hiyo kumshukuru kwa kazi yote iliyofanywa na wafanyakazi wa afya.

"Ninyi ni mashujaa na tunawaenzi sana," alisema kabla ya kuwaambia waandishi wa habari: "Ninafanya hivi kuonyesha kuwa watu wanapaswa kuwa tayari kupata chanjo wakati itakapopatikana, wasiwi na hofu yoyote. "

Wakati Marekani inakabiliwa na mlipuko wa pili ambao unaendelea kusababisha vifo vingi, Joe Biden alitoa wito kwa Wamarekani kuheshimu hatua za usafi, na kuepuka kusafiri wakati wa sikuu za Krismasi na mwaka mpya.

" Huu ni mwanzo tu. Ni jambo muhimu kupata chanjo. Lakini itachukua muda. Na kwa sasa, natumai watu watawasikiliza wataalam. vaeni barakoa, kaaeni mbali baina yenu. Hii ni muhimu sana kwa sababu bado tunakabiliwa na janga hili baya kabisa ".

Biden amekuwa akisema baada ya kuingia madarakani, serikali yake itatoa chanjo Milioni 100 kwa siku 100 za Kwanza madarakani.

UINGEREZA

Boris Johnson: Ninaelewa hatua ya mataifa ya kigeni dhidi ya Uingereza

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson, amesema anaelewa hatua ya mataifa ya kigeni kusitisha safari zake za ndege nchini humo kutokana na nchi hiyo kushuhudia kuenea kwa haraka kwa aina mpya ya virus vya Corona.

Mataifa zaidi ya 40 yamesitisha safari za ndege kati yao na Uingereza, wakati huu viongozi wa Umoja wa Ulaya wakitarajiwa kuja na mkakati mmoja wa kupambana na janga hili.

 

Nchi zilizojiunga na orodha na mataifa kadhaa ya Ulaya ni pamoja na Kuwait, Tunisia, Urusi, Oman, Saudi Arabia pamoja na Chile. Nchi nyingine ni Israel, El Salvador, Morocco, India, Jordan na Argentina. Mbali na Uingereza, nchi hizo zimezuia pia ndege kutoka na kwenda Afrika Kusini na Denmark, ambako kuna virusi vipya vilivyogundulika

 

Waziri wa Usafiri wa Ufaransa, Jean-Baptiste Djebbari, amesema maafisa wanatarajia kuanzisha hatua za usafi barani Ulaya katika muda wa saa chache zijazo ambazo zitaruhusu usafiri kutoka Uingereza kuanza tena.

 

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas amesema kwamba vizuizi vya usafiri vimewekwa katika juhudi za kuepusha hali ya kutodhibitika kwa virusi hivyo, lakini hilo sasa linaratibiwa na nchi wanachama 27 za Umoja wa Ulaya.

 

Wakati huo huo Shrika la Afya Duniani, WHO, limetahadharisha dhidi ya wasiwasi wa kupindukia kuhusu aina mpya ya virusi vya Corona vinavyosamba kwa kasi kubwa, baada ya kugunduliwa nchini Uingereza na baadae Afrika Kusini.

 

Maafisa wa WHO wamesema hawana ushahidi wowote unaoonyesha kwamba aina hiyo mpya ya virusi inawafanya watu kuwa wagonjwa zaidi au kuwa ni mbaya zaidi kuliko virusi vilivyokuwepo awali vya ugonjwa wa COVID-19. Ingawa WHO imethibitisha kwamba aina hiyo mpya inaonekana kuenea kwa kasi zaidi.

 

Uingereza ina mamabukizi zaidi ya Milioni mbili, huku watu wengine zaidi ya Elfu 67 wakipoteza maisha.

 

KENYA

 

Madakati wanaendelea na mgomo wao kwa siku ya pili nchini Kenya

 

Madaktari wanaofanya kazi kwenye hospital za umma nchini Kenya, kwa siku ya pili leo, wanaendelea na mgomo wao kulalamikia kutopewa bima ya afya na ukosefu wa vifaa vya kujikinga wanapowatibu wagonjwa wa janga la COVID-19.

 

Mgomo huu unakuja wakati huu nchi nchi hiyo inapoendelea kukabiliana na janga la Corona.

 

Serikali ya Kenya kupitia Waziri wa afya Mutahi Kagwe imetishia kuwafuta kazi madaktari na wahudumu walioamua kugoma.

 

Kufikia sasa Kenya imerekodi visa 94,614 vya maambukizi ya virusi vya Corona baada ya visa vipya 114 kuthibitishwa na vifo 1,644 baada ya watu wengine 5 kuthibitishwa kufariki dunia kutoka na janga hilo hatari la COVID-19.

 

Watu 325 wameripotiwa kupona virusi hivyo na kufanya idadi ya jumla ya watu waliopona kufikia 76,060.