MAREKANI

Trump asaini muswada kuhusu misaada ya COVID-19

Donald Trump, rais wa Marekani
Donald Trump, rais wa Marekani REUTERS/Carlos Barria

Hatimaye rais wa Marekani Donald Trump ametia saini muswada wa sheria wa dola bilioni 900, unaolenga kusaidia watu walioathiriwa na ugonjwa hatari wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya Corona.

Matangazo ya kibiashara

Donald Trump, ambaye atakabidhi madaraka mnamo Januari 20 kwa mpinzani wake kutoka chama cha Democratic Joe Biden, amebadilisha uamuzi wake wa kuzuia muswada uliopitishwa wiki iliyopita na Bunge la Congress baada ya kushinikizwa na wabunge kutoka pande zote.

Rais alikuwa ameomba misaada ya moja kwa moja kwa familia zilizo na shida iongezwe kutoka dola 600 hadi dola 2,000.

Chanzo kilio karibu na faili hiyo kimesema kwamba washauri wengine wa Donald Trump walikuwa wamemsihi atie saini kwenye muswada huo, wakisema kuwa hawaoni sababu ya kuupinga.

Wabunge kutoka chama cha Democratic wamependekeza kuongeza misaada ya moja kwa moja kwa Wamarekani hadi dola 2,000 kutoka dola 600 ambazo zinabainishwa kwa sasa katika muswada huo kama sehemu ya mpango wa kukuza uchumi, na kujibu moja ya madai ya Donald Trump.

Lakini wabunge wa chama cha Republican wamekataa pendekezo hilo, ambalo wanaona ni lenye gharama kubwa.

Mabadiliko haya yanakuja wakati wabunge wa chama cha Rarepublican wengi wamekataa kurudi kwenye pendekezo ambalo walikuwa wamepigia kura.

Kiongozi wa wengi katika Bunge la Seneti Mitch McConnell amesema "anampongeza rais kwa kutia saini kwenye muswada huo."

Spika wa Bunge Nancy Pelosi amesema: "rais lazima sasa atoe wito kwa wabunge wa chama cha Rarepublican katika bunge la Congress kufuata mfano wake na kuunga mkono kuongezwa kwa kiwango cha dola 2,000."