MAREKANI

Mazungumzo ya siri ya Trump kujaribu kubadilisha uchaguzi Georgia yanaswa

Donald Trump, rais wa Marekani
Donald Trump, rais wa Marekani MANDEL NGAN / AFP

Rais wa Marekani anaye maliza muda wake Donald Trump amesikika akimtaka afisa wa uchaguzi 'kumtafutia kura 11,780' kuwezesha kubadilishwa kwa matokeo ya uchaguzi katika jimbo la Georgia.

Matangazo ya kibiashara

Katika kanda ya sauti iliyotolewa na Gazeti la Washington Post , rais Trump anasikika akimuambia kamishna wa uchaguzi katika jimbo la Georgia Brad Raffensperger, kumtafutia kura 11,780, ambazo zingeweza kubadilisha matokeo na kumpokonya ushindi rais mteule Joe Biden katika jimbo hilo la Kusini mashariki.

"Nataka tu kupata kura 11,780," Bwana Trump alimwambia katibu wa chama cha Republican Brad Raffensperger jimboni humo katika mazungumzo yaliyorekodiwa na kutolewa na gazeti la Washington Post.

Hata hivyo Bw. Raffensperger anasikika akijibu kuwa matokeo ya uchaguzi ya Georgia yalikuwa sawa.

Kuchapishwa kwa mazungumzo hayo na gazeti la Washington Post ni ufichuzi wa juhudi nyingine ambazo Trump amekuwa akizifanya kwa miezi miwili iliyopita, kutaka kuwaaminisha watu kuwa kushindwa kwake na Joe Biden kulitokana na hila za wizi wa kura.

Madai hayo ya udanganyifu katika uchaguzi ambayo yanaendelezwa na Rais Donald Trump na washirika wake yametupiliwa mbali na maafisa wa uchaguzi wa majimbo na kesi zao nyingi zimetupwa nje na mahakama.

Joe Biden alishinda uchaguzi wa Georgia pamoja na majimbo mengine muhimu na kumuwezesha kupata kura 306 za wajumbe dhidi ya Bwana Trump aliyepata kura 232.