MAREKANI

Marekani: Warnock kutoka chama cha Democratic ashinda katika uchaguzi muhimu wa maseneta Georgia

Raphael Warnock, mshindi wa kiti cha Senate katika jimbo la Georgia nchini Marekani
Raphael Warnock, mshindi wa kiti cha Senate katika jimbo la Georgia nchini Marekani BRANDON BELL / GETTY IMAGES

Mgombea wa wa chama cha Democratic Raphael Warnock ameibuka mshindi katika uchaguzi wa maseneta dhidi ya mgombea wa chama cha Republican Kelly Loeffler katika jimbo la Georgia, kulingana na vituo vya habari vya CNN, CBS na NBC leo Jumatano, Januari 6.

Matangazo ya kibiashara

Raphael Warnock, mchungaji wa kanisa huko Atlanta ambapo Martin Luther King alifanya kazi, ataandika historia kwa kuwa seneta wa kwanza mweusi aliyechaguliwa katika jimbo hili la kusini.

Chama cha Democratic kinatarajia kushinda uchaguzi mwingine mdogo wa maseneta katika jimbo la Georgia kuchukua udhibiti wa Bunge la Seneti, suala kubwa.

Hili ni suala kubwa kwa utawala wa Joe Biden, ambaye atakabidhiwa madaraka Januari 20.

Donald Trump alikuja kuwaunga mkono maseneta wawili kutoka chama cha Republican wanaomaliza muda wao ambao wanawania nafasi zao katika Bunge la Seneti Jumanne hii, Januari 5.

Donald Trump anaendelea na msimamo wake wa kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi mpinzani wake kutoka chama cha Democratic, Joe Biden.

"Nilishinda Georgia", "hatuwezi kupoteza Georgia", "huu ni uchaguzi uliogubikwa na udanganyifu mkubwa". Haya ni maneno yake ya kwanza Jumatatu hii jioni alipofika jukwaani.

Hata hivyo, matokeo ya kura yalihesabiwa mara kadhaa huko Georgia na ni wazi: Joe Biden ndiye ambaye alishinda uchaguzi wa urais na ndiye ambaye alishinda katika jimbo hili kwa kura 12,000 dhidi ya Donald Trump.

Siku ya Jumatatu hii jioni, Donald Trump alimshambulia gavana wa jimbo la Georgia, ambaye ni mmoja wa wafuasi wake wa zamani na kamishna wa uchaguzi katika jimbo la Georgia Brad Raffensperger, ambaye anamshinikiza kubadili matokeo.

"Watu wasio na uwezo", amemshutumu Trump. Katika hotuba yake yote, rais aliendelea kutoa habari za uwongo, akibaini kwamba uchaguzi uligubikwa na udanganyifu mkubwa, na kusema kulikuwepo na wapiga kura hewa.