MAREKANI

Shughuli za Bunge la Congress zaendelea baada ya machafuko Capitol Hill

Wafuasi wa rais Donald Trump wakiandamana katika eneo la Capitol Hill
Wafuasi wa rais Donald Trump wakiandamana katika eneo la Capitol Hill AP Photo/Julio Cortez

Bunge la Congress la Marekani limeendelea na kikao cha kuidhinisha ushindi wa urais mteule Joe Biden. Kikao hicho kilikuwa kimekatizwa kwa saa kadhaa baada ya waandamanaji wanaomuunga mkono Donald Trump kuvamia majengo ya Capitol Hill na kusababisha vurugu.

Matangazo ya kibiashara

Hotuba ya Donald Trump ya kuwataka wafuasi wake kujielekeza mbele ya majengo ya Capitol Hill inasadikiwa kuwa ndio imechochea uvamizi huo.

Polisi katika eneo la Capitol walijibu maandamano hayo kwa kutumia bunduki na gesi ya kutoa machozi wakati mamia ya waandamanaji walipovamia na kutaka kulilaazimisha bunge kubatilisha ushindi wa Biden dhidi ya rais Donald Trump, muda mfupi baada ya Warepublican wenzake na Trump kuanzisha juhudi ya dakika za mwisho kutupilia mbali matokeo ushindi wa Biden.

Donald Trump aliwahimiza wafuasi wake waende Capitol wakati wa mchakato wa kuidhinisha ushindi wa Joe Biden. Mamia ya waandamanaji wanaomuunga mkono Trump waliandamana nje ya Bunge na kuingia ndani ya jengo hilo , na kusababisha kusitishwa kwa kikao na kuondolewa kwa maseneta ndani ya jengo hilo.

Polisi imechukua karibu saa nne kurejesha hali ya utulivu katika jengo hiulo baada ya kutumwa kwa vikosi vya walinzi wa kitaifa. Karibu saa 8 jioni kwa saa za Marekani, maseneta hatimaye waliweza kuanza tena kikao cha kuidhinisha ushindi wa Joe Biden.

Mwanamke mmoja alipigwa risasi na kuuawa ndani ya jengo la Capitol Hill baada ya afisa wa polisi kurusha risasi.

Waandamanaji wasiopungua 13 wamekamatwa na polisi. Kwa sasa Washington iko chini ya sheria ya kutotoka nje kuanzia saa 12 jioni hadi saa 12 asubuhi kwa saa za Marekani.