MAREKANI

Shinikizo dhidi ya rais Trump zaendelea, polisi afariki dunia

Maandamano katika eneo la Capitol Hill
Maandamano katika eneo la Capitol Hill REUTERS/Daniel Acker

Brian Sicknick afisa wa polisi katika eneo la Capitol Hill kuliko majengo ya Bunge la wawakilishi na Senate, kulikotokea vurugu zilizosabishwa na wafuasi wa rais Donald Trump, amefariki dunia kutokana na majereha aliyoyapata wakati akipambana na waandamanaji.

Matangazo ya kibiashara

Kifo hiki kimechochea viongozi wakuu wa chama cha Democratic, wanaotaka rais Trump kuondolewa madarakani kwa kuchochea vurugu hizo.

Spika wa bunge la wawakilishi Nancy Pelosi, amemtaka Makamu wa rais Mike Pence kutumia kifungu nambari 25 cha katiba, kutangaza kuwa rais Trump hana uwezo wa kuendelea kuwa kiongozi wa nchi hiyo.

Iwapo Pence, ataamua kutumia kifungu hicho, atahitaji uungwaji mkono wa Mawaziri wanane kufanikisha mpango huo lakini hilo huenda lisifanyike kwa sababu ya muda mfupi unaosalia kwa Trump kuwa madarakani.

Aidha, Pelosi amesema kuwa mwenyewe ataanzisha harakati za kumwondoa madarakani rais Trump ambaye ataondoka uongozini tarehe 20 mwezi huu.

Machafuko hayo yaliyotokea siku ya Jumatano, wakati Maseneta walipokuwa wanakutana kujadili na kuidhinisha matokeo yaliyompa ushindi rais mteule Joe Biden baada ya uchaguzi wa urais uliofanyika mwewi Novemba, yamesababisha vifo vya watu watano na wengine kujeruhiwa.