UCHAGUZI NICARAGUA

Upinzani walaani mateso dhidi ya wafuasi wake

Maandamano ya kumuunga mkono Daniel Ortega rais wa Nicaragua
Maandamano ya kumuunga mkono Daniel Ortega rais wa Nicaragua ©REUTERS/Oswaldo Rivas

Viongozi wa upinzani nchini Nicaragua wanashutumu serikali au wafuasi wa serikali ya Rais Daniel Ortega kwa visa vya untantasaji na mateso dhidi ya wafuasi wao.

Matangazo ya kibiashara

Rais Daniel Ortega anatarajiwa kuwania muhula wa nne mfululizo wa miaka mitano mnamo mwezi Novemba mwaka huu.

Angalau viongozi 52 wa upinzani walifanyiwa "mateso, unyanyasaji, uvamizi, kukamatwa, kuibiwa na kuwekwa kizuizini" mnamo mwaka 2020, vitendo ambavyo upinzani unadai kuwa vilitekelezwa na polisi au wafuasi wa utawala, kulingana na ripoti iliyowasilishwa na muungano wa upinzani wa UNAB.

UNAB inaundwa na mashirika ya kiraia na mashirika ya haki za binadamu na vile vile vyama vya siasa ambavyo haviwakilishwi bungeni.

Kulingana na ripoti hiyo, iliyoitwa "Nicaragua inayokabiliwa na ukiukwaji wa haki", "viongozi kadhaa (wa upinzani) wanashikiliwa kiholela na polisi katika vifungo vya nyumbani kote nchini bila hata hivyo kufunguliwa kesi yoyote mahakamani ".

Msemaji wa UNAB Josué Garay alitolea mfano wa kesi ya viongozi wa upinzani ambao nyumba zao zimezingirwa na maafisa wa polisi ambao huwazuia kutoka hata kwenda kuonana na daktari au kwenda kwa duka la dawa.

Wapinzani mia moja na ishirini wanaotuhumiwa kuhusika katika maandamano ya mwaka 2018 ya kutaka rais Ortega ajiuzulu kwa sasa wako jela, kulingana na ripoti hiyo, ambayo inabainisha kuwa miongoni mwa wafungwa hao, 64 walikamatwa mnamo mwaka 2020.

Maandamano hayo yalizimwa baada ya ukandamizaji uliosababisha vifo vya watu 320, kulingana na mashirika ya haki za binadamu, wakati maelfu ya Wanicaragua walilazimika kuyatoroka makaazi yao na kukimbilia nje ya nchi.