MAREKANI

Hatma ya Donald Trump mashakani, baada ya wabunge kuazimia kumfunfungulia mashitaka

Rais wa Marekani Donald Trump
Rais wa Marekani Donald Trump AP Photo/Ross D. Franklin

Rais wa Marekani Donald Trump anatarajiwa kushtakiwa kwa kuchochea machafuko katika makao makuu ya Bunge la Seneti, baada ya bunge kupiga kura ya kutokuwa na imana naye Jumatano wiki hii.

Matangazo ya kibiashara

Wabunge wa chama cha Democrat waliungwa mkono na wabunge 10 kutoka chama cha Republican kwa kupitisha kura hiyo ya kumshtaki rais kwa sauti 232 dhidi ya wabunge 197 waliopinga hatua hiyo.

Ni kwa mara ya pili Bunge la Congress kupiga kura ya kutokuwa na imani na rais Donald Trump na kushtakiwa kwa makosa ya uhalifu.

Rais huyo alituhumiwa na bunge la Congress kwa kuchochea ghasia ziizosababisha uvamizi wa Jumba la bunge la Capitol kufuatia hotuba yake aliyotoa tarehe sita mwezi Januari katika mkutano wa hadhara nje ya Ikulu ya Whitehouse.

Aliwataka wafuasi wake kuandamana kwa amani na uzalendo ili sauti zao zisikike, lakini pia kukabiliana na uchaguzi ambao alidai kwamba ulikumbwa na udanganyifu mkubwa.

Donald Trump ni rais wa kwanza katika historia ya Marekani kupigiwa kura ya kutokuwa na imani mara mbili ama kushtakiwa kwa makosa ya uhalifu na bunge hilo la Congress.

Iwapo Bwana Trump atapatikana na hatia huenda akapigwa marufuku kushikilia wadhfa wowote wa ofisi ya umma.

Wakati huo huo wanajeshi wengi wamepelekwa katika mjii mkuu wa Marekani, Washington, kuimarisha ulinzi, siku sita kabla ya kuapishwa kwa Joe Biden kuwa rais rasmi wa taifa hilo lenye nguvu duniani, baada ya kushinda uchaguzi wa Novemba 2020.

Hata hivyo Shirika la kijasusi nchini Marekani FBI limeonya kwamba kuna uwezekano wa kuzuka kwa maandamano katika majimbo yote 50 kabla ya kuapishwa kwa rais mteule Joe Biden wiki ijayo.