MAREKANI

Majimbo yote 50 ya Marekani yamewekwa katika hali ya tahadhari kueekea kuapishwa Joe Biden

Rais mteule wa Marekani Joe Biden
Rais mteule wa Marekani Joe Biden AP Photo/Andrew Harnik

Makundi kadhaa ya waandamanaji wamejikusanya katika majumba ya serikali nchini Marekani, wengine wakiwa wamejihami kwa silaha, hali ya wasi wasi ikizidi kutanda wiki chache baada ya vurugu kushuhudiwa katika jumba la bunge la waakilishi la Capital Hill, ambapo watu watano walipoteza maisha na wengine kupata majeraha.

Matangazo ya kibiashara

Maandamano hayo yanashuhudiwa katika majimbo ya Texas, Oregon, Michigan, Ohio na kwingineko. Shirika la ujasusi nchini humo FBI limeonya uwezekano wa uwepo wa waandamanaji wenye silaha kuelekea kuapishwa kwa rais mpya wa Marekani Joe Biden Jumatano wiki hii.

Majimbo yote 50 ya Marekani yamewekwa katika hali ya tahadhari kutokana na uwezekano wa maandamno ya ghasia, kabla ya kuapishwa kwa rais mteule Joe Biden siku ya Jumatano.

Eneo kubwa la Washington DC litafungwa kabla ya sherehe ya kuapishwa kwa Joe Biden huku maelfu ya maafisa wa kikosi cha ulinzi wa kitaifa wakisambazwa kila mahali.

Barabara nyingi - nyengine zikiwa mbali na majengo ya Bunge , eneo la ghasia mbaya za tarehe sita Januari - yamezuiwa na vizuizi na ua wa chuma.

Wakati huohuo, kundi la Biden limeweka mipango kufutilia mbali baadhi ya sera zilizoweka na rais Trump.

Muda mfupi baada ya Joe Biden kuingia katika Ikulu ya Whitehouse , ataanza kubadili baadhi ya maagizo yaliowekwa na Trump kama njia ya kuonesha tofauti kati ya utawala unaoondoka na unaoingia , kulingana na barua ilioonekana na vyombo vya habari vya Marekani.