GUATEMALA

Msafara wa wahamiaji kutoka Honduras wazuia kikatili

Wahamiaji kutoka Honduras
Wahamiaji kutoka Honduras Johan ORDONEZ / AFP

Msafara wa wahamiaji, ambao uliondoka Honduras Ijumaa kuelekea Marekani, umezuiliwa tangu Jumapili, Januari 17 nchini Guatemala, ambapo mamlaka imeweka vizuizi barabarani ili kudhibiti watu kuitoroka nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Jumapili hii, kundi la maelfu ya watu ambao walijaribu kuvuka kituo cha kijeshi walirudishwa nyuma kwa nguvu.

Vikosi vya usalama na ulinzi vilitumia gesi ya kutoa machozi, huku wahamiaji kadhaa wakichapwa vibaya marungu.

Kikundi cha wanajeshi na maafisa wa polisi walifunga barabara , na kuwazuia wengi wao kuendelea na safari.

Baadhi ya wahamiaji hao bado walilazimisha kwa nguvu kupita, na kuwafanya maafisa wa usalama kuwasukuma nyuma.

Wahamiaji wanaokadiriwa kuwa 7,000 , wengi wao kutoka Honduras, wameingia katika siku za hivi karibuni, wakikimbia umasikini na ghasia.

Kila mwaka, maelfu ya wahamiaji wa Amerika ya kati hujaribu safari hii ili kujaribu kufika Marekani, mara nyingi hutembea kwa miguu.

Rais mteule wa Marekani Joe Biden, ambaye atakabidhiwa madaraka Januari 20, ameapa kuondoa sera kali za uhamiaji zilizowekwa na mtangulizi wake, Donald Trump.

Hata hivyo utawala umewaonya wahamiaji kutofanya safari , kwa sababu sera za uhamiaji hazitabadilishwa haraka.

Karibu watu 9,000 kutoka Honduras waliondoka nchini mwao wiki iliyopita na kujiunga na msafara huu.

Lakini maelfu miongoni mwao tayari wamerudishwa nyumbani. Wale ambao wamebaki wanatarajiwa wiki hii kwenye mpaka wa Mexico na kupokelewa na msururu wa askari wa kikosi cha walinzi wa kitaifa na maafisa wa uhamiaji.