Dunia yasubiri kuapishwa kwa Joe Biden
Imechapishwa:
Joe Biden anatarajiwa kuapishwa kuwa rais wa 46 wa Marekani saa chache zijazo katika eneo la capitol Hill jijini Washington DC katika hafla ambayo inasubiriwa kote duniani.
Biden mwenye umri wa miaka 78 anatarajiwa kuapishwa na makamu wake Kamala Harris, mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo katika historia ya Marekani.
Kinyume na miaka iliyopita wakati sherehe hizi zilishuhudia umati mkubwa wa watu, wakati huu, kutakuwa na watu wachache kutokana na janga la Corona, linaloitesa nchi hiyo.
Usalama umeimarishwa jijini Washington DC hasa katika eneo la Capitol Hill, ambako kuna wanajeshi zaidi ya Elfu 25, hatua ambayo imechukuliwa baada ya wafuasi wa rais anayeondoka madarakani Donald Trump kuzua vurugu mapema mwezi huu katika majengo ya bunge.
Trump ambaye aliondoka katika Ikulu ya White House saa chache kuelekea kuapishwa kwa Biden, kwenda nyumbani kwao katika jimbo la Florida, anakuwa rais wa nne katika histori ya nchi hiyo kutohudhuria kuapishwa kwa mrithi wake.
Hakutakuwa na shamrashamra zozote katika sherehe hiyo ambayo pia itahudhuriwa na maraius wa zamani Barack Obama, George Bush, Bill Clinton na wake zao pamoja na viongozi wa juu wa bunge la wawakilishi na senate.
Baada ya kuapishwa kwake, Biden anatarajiwa kutoa hotuba yake ya kwanza kama rais wa nchi hiyo huku akieleza ajenda yake kubwa itakuwa ni kupambana na janga la Corona na kuwaunganisha raia wa nchi hiyo ambao wamegawanyika baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.