MAREKANI-MEXICO

Mexico yakaribisha hatua ya Biden kusitisha ujenzi wa ukuta wa mpaka

Wahamiaji kutoka Amerika Kusini
Wahamiaji kutoka Amerika Kusini Ueslei Marcelinov/Reuters

Serikali ya Mexico imekaribisha hatua ya rais mpya wa Marekani Joe Biden ya kusitisha ujenzi wa ukuta kwenye mpaka wake na Marekani, pamoja na muswada wake unaohusiana na mageuzi ya sheria ya uhamiaji.

Matangazo ya kibiashara

Rais wa Mexico Andrès Manuel López Obrador, AMLO, amekabribisha hatua hiyo.

 

"Hii ni hatua mpya ya kuheshimiana na yenye matumaini kutoka pande zote mbili," ni kauli ya serikali ya Mexico inayoelezea uhusiano wa baadaye na Joe Biden.

 

 

Mwezi Januari 2017 Donald Trump alitia saini amri ya rais kuidhinisha kuanza kujengwa ukuta katika mpaka kati ya Marekani na Mexico. Amri hiyo ililenga kutimiza mojawapo ya ahadi kuu za Trump alizozitoa wakati wa kampeni zake za uchaguzi. Wakati huo Trump alisema “nchi isiyokuwa na mipaka sio nchi”.

 

Sehemu ya mpaka huo kati ya Marekani na Mexico ulikuwa uliwekewa uzio lakini Trump alisema ukuta unahitajika kuwazuia wahamiaji haramu kutoka nchi hiyo ya Amerika ya kusini kuingia Marekani na pia kuagiza ukaguzi wa mipaka kukamilishwa katika kipindi cha siku 180.

 

Mwaka 2016, Trump alisema lengo la ukuta huo ni kuwazuia wahamiaji kutoka Mexico kuingia Marekani kwani huleta matatizo mengi yakiwemo dawa za kulevya, uhalifu na ubakaji. Wakati huo alibaini kwamba gharama ya ukuta huo iliyotarajiwa kuwa ya mabilioni ya dola itagharamiwa na Mexico, suala ambalo serikali ya Mexico ilipinga vikali.

 

Wamexico zaidi ya milioni kumi wanaishi bila kibali chochote nchini Marekani kwa miaka mingi.