MAREKANI-JOE BIDEN

'Nitakuwa rais wa Wamarekani wote': Joe Biden atoa wito kwa Wamarekani kuwa na umoja

Rais wa Marekani, Joe Biden
Rais wa Marekani, Joe Biden REUTERS/Brendan McDermid

"Najua tofauti zinazotugawanya ni za kina na za kweli," amesema Joe Biden katika hotuba yake ya kwanza kama Rais wa 46 wa Marekani, kabla ya kutoa wito wa umoja kwa Wamarekani.

Matangazo ya kibiashara

"Demokrasia ni yenye thamani, demokrasia ni kitu ambacho kwa muda wowote kinaweza kuvunjika, na leo marafiki zangu, demokrasia imeshinda," Joe Biden amesema katika hotuba yake ya kuapishwa, akitoa wito kwa umoja. Katika hotuba ya dakika 20, Rais wa 46 wa Marekani pia aliahidi kuwa "rais wa Wamarekani wote."

 

Kuhusu vita dhidi ya COVID-19, ambayo imeua zaidi ya watu 400,000 nchini Marekani, rais aliomba Wamarekani kuweka kando tofauti zao ili kukabiliana na "majira ya baridi kali" ambayo yanakuja katika "kipindi kigumu zaidi na hatari ”cha janga la COVID-19.

"Lazima tuachane na vita hivi vinavyotaka kutuangamiza"

 

Kwa upande wa kisiasa, Joe Biden amejaribu kuunganisha uhusiano wa Amerika mbili zilizogawanyika. “Suluhisho sio kukabiliana na tatizo mwenyewe. Lazima tuachane na vita hivi vya wenyewe kwa wenyewe kati ya Wekundu na Bluu, ”alisema.

 

Ishara ya mgawanyiko huu, rais anayemaliza muda wake Donald Trump, ambaye hakuhudhuria katika hafla ya kuapishwa kwa rais mpya na alikataa kukubali kushindwa katika uchaguzi wa mwezi Novemba 2020 na kusema kuwa uchaguzi uligubikwa na udanganyifu mkubwa.

 

Kipindi cha maandalizi ya kukabidhiana madaraka kati ya utawala wa Trump na Biden kiligubikwa sana na matukio ya kihistoria, kama vile kitendo cha wafuasi wa Donald Trump kuvamia majengo ya bunge la Seneti, Capitol Hil Januari 6. Kutokana na mfarakano huu ambao umewagawanya Wamarekani, Joe Biden ametoa wito kwa raia "kuanza tena kufanya kazi pamoja, kutusikia, kutuheshimu". "Maisha ya kisiasa hayana haja ya kuwa kama moto ambao huharibu kila kitu sehemu unakopia," amesema.

 

"Kwa umoja tunaweza kufanya mambo makubwa"

 

Bila kumtaja mtangulizi wake, rais mpya amewataka Wamarekani kufutilia mbali madai yasio kuwa na msingi, akimaanisha Donald Trump ambaye ameshtumu udanganyifu mkubwa uliogubika uchaguzi, bila hata hivyo kutoa ushahidi wowote.

 

“Sio tofauti zote zinapaswa kusababisha vita. (…) Kuna ukweli na kuna uwongo, uongo unaosemwa kwa kutafuta manufaa. Na kila mmoja wetu ana jukumu na anahusika, kama raia, kama Wamarekani, na haswa kama viongozi, (...) kutetea ukweli na kupambana dhidi ya uwongo, " ameongeza.

 

Joe Biden pia ameonyesha utayari wake wa "kushinda" "ubaguzi" na "ugaidi wa ndani". "Kwa umoja tunaweza kufanya mambo makubwa, kushinda virusi hivi, kupambana na ubaguzi wa rangi na kuifanya Marekani kuwa tena nchi yenye nguvu zaidi duniani," amebaini rais Joe Biden.