MEXICO-COVID 19

Rais wa Mexico Lopez Obrador apatikana na virusi vya Corona

Rais wa Mexico  Andrés Manuel Lopez Obrador
Rais wa Mexico Andrés Manuel Lopez Obrador Mexican Presidency / AFP

Rais wa Mexico Andres Manuel Lopez Obrador, mwenye umri wa miaka 67, ametangaza kwamba amefanya vipimo na kupatikana na virusi vya Corona, akibaini kwamba anaonesha dalili za kawaida.  Amesema ana matumaini ya kupata nafuu na ataendelea na shughuli za kila siku za kuongoza taifa.

Matangazo ya kibiashara

“Ninasikitika kuwafahamisha kuwa nimeambukizwa virusi vibavyosababisha ugobjwa wa COVID-19. Ninaendelea vizuri, na nimeanza kupewa matibabu, "rais  Andres Manuel Lopez Obrador amesema kwenye akaunti yake rasmi ya Facebook.

Bwana Lopez Obrador, ambaye aliagiza raia wake kuendelea kufanya shughuli zao mbalimbali wakati wa janga hilo, amemteua Katibu wa Mambo ya Ndani Olga Sánchez kuchukua nafasi yake katika mkutano wake na waandishi wa habari Jumatatu hadi Ijumaa saa moja asubuhi kwa saa za Mexico.

"Nitakuwa mwangalifu kwa maswala ya umma kutoka Ikulu ya kitaifa. Kwa mfano, [Jumatatu], nitafanya mahojiano kwa njia ya simu na rais Vladimir Putin, ”Lopez Obrador amesema, akimaanisha mwenzake wa Urusi.

Kiongozi huyo wa mrengo wa kushoto alikuwa na hafla tatu za umma mwishoni mwa wiki, ya mwisho ilikuwa siku ya  Ijumaa asubuhi katika jimbo la San Luis Potosí.

Wakuu wengine wa nchi na serikali ambao walipatikana na virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa hatari wa COVID-19, ni Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson na Marais wa Brazil Jair Bolsonaro, Marekani Donald Trump na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.

Andres Manuel Lopez Obrador havai barakoa katika maeneo ya umma. Alionekana tu akivaa barakoa wakati wa aliposafiri kwa ndege.

Rais wa Mexico Andres Manuel Lopez anafahamika kwa kupuuza kitisho cha janga la virusi vya Corona.

Mexico imepoteza zaidi ya watu 149,000 kutoka na ugonjwa wa COVID-19 na kuwa taifa la nne duniani kwa idadi kubwa ya vifo tangu kuzuka kwa janga hilo mwishoni mwa mwaka 2019.