MAREKANI-CHINA

Marekani kuendelea kutoza kodi bidhaa kutoka China

Rais wa Marekani Joe Biden
Rais wa Marekani Joe Biden AP Photo/Andrew Harnik

Marekani itaendelea kwa sasa na kutekeleza sheria iliyowekwa na utawala wa Donald Trump, inayotoza kodi bidhaa kutoka China zenye thamani ya mabilioni ya dola, Waziri wa Fedha wa Marekani Janet Yellen amesema.

Matangazo ya kibiashara

Hata hivyo Janet Yellen amebaini kwamba Washington itaamua hatua itakazo chukuwa ya baada ya kutathimini kwa uangalifu.

Akiongea kwenye mahojiano na kituo cha CNBC, Janet Yellen ameongeza kuwa utawala mpya wa Marekani unaitaka China kuheshimu ahadi zilizotolewa katika suala la biashara, hasa kwa kuzingatia makubaliano yaliyotiwa saini na mataifa mawili makubwa kichumi duniani mapema mwaka 2020.

"Kwa sasa, tutaendelea kutekeleza sheria iliyowekwa na utawala wa Donald Trump inayotoza kodi bidhaa kutoka China [...] na baada ya muda tutatathmini kile tunachokiona kuwa sahihi," amesema

Alipoulizwa ikiwa kodi hii imezaa matunda, Janet Yellen amesita, kisha akajibu, "Tutaangalia."

Ikulu ya White House ilibaini mwezi uliopita kwamba itapitia hatua zote za usalama wa kitaifa zilizoamuliwa na Donald Trump, ambapo mkataba wa kibiashara wa "awamu ya 1" kati ya Washington na Beijing ulisainiwa na rais wa zamani.

Mkataba huo ulipunguza mvutano kati ya China na Marekani baada ya miezi kadhaa ya vita vya biashara, lakini hatua zilizochukuliwa na nchi hizo kutoza kodi bidhaa kutoka nchi mojawapo zimeendelea kutekelezwa na nchi hizo tangu wakati huo.

Joe Biden, ambaye hivi karibuni alielezea nia yake ya kurekebisha uhusiano na washirika wa Washington, amechukua hatua kali kwa Beijing, ikiwa ni pamoja na wiki hii akionya kuwa China itapata madhara kutokana na ukiukwaji wa haki za binadamu.