MAREKANi-SIASA

Marekani: Trump kupeperusha bendera ya chama cha Republican 2024

Aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump akizungumza katika mkutano wa CPAC, huko Orlando, Florida Februari 28, 2021.
Aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump akizungumza katika mkutano wa CPAC, huko Orlando, Florida Februari 28, 2021. REUTERS - OCTAVIO JONES

Aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump ameweka wazi uwezekano wa kuwania tena kwenye kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2024. na kumshambulia mrithi wake Joe Biden, kutoka chama cha Democratic huku akirejelea madai yake yasio kuwa na msingi kwamba aliibiwa uchaguzi wa mwezi Novemba 2020.

Matangazo ya kibiashara

Akionekana kwa mara ya kwanza kwa umma tangu aondoke madarakani, karibu wiki sita zilizopita, Donald Trump alionyesha nia yake ya kupeperusha bendera ya Chama cha Republican katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2024;

Akizungumza katika mkutano wa kisiasa wa muungano wa kihafidhina CPAC, Conservative Political Action Conference, uliofanyika mjini Orlando katika jimbo la Florida, Donald Trump alisema huenda akajitosa katika kinyang'anyiro cha urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Trump anadai kuwa uchaguzi wa mwezi Novemba ulikumbwa na udanganyifu mkubwa lakini hajawahi kutoa ushahidi wowote kuunga mkono madai yake.

Trump pia alikataa wito wa kuanzishwa kwa chama kipya cha kisiasa.