COLOMBIA-FARC-USALAMA-SIASA

Colombia: Waasi kumi wauawa katika mashambulizi ya anga ya jeshi

Wanajeshi wa Colombia wakifanya mazoezi.
Wanajeshi wa Colombia wakifanya mazoezi. Raul ARBOLEDA AFP/Archivos

Wapiganaji kumi wa zamani wa kundi la waasi la FARC wameuawa na wengine watatu wamekamatwa katika shambulio la anga lililotekelezwa na jeshi la Colombia katika mkoa wa Guaviare, kusini mashariki mwa nchi, Waziri wa Ulinzi Diego Molano Molano amesema.

Matangazo ya kibiashara

Wapiganaji hawa walipinga makubaliano ya amani yaliyosainiwa mnamo mwaka 2016 kati ya kundi la waasi la FARC na serikali.

"Wakati wa operesheni hiyo iliyoendeshwa na vikosi vyetu vya ulinzii, kwa msaada wa ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali, wapiganaji 13 wa zamani wa kundi la FARC wanaoongozwa na mtu anayejulikana kwa jinala Gentil Duarte wameangamizwa," Diego Molano ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Wapiganaji hao wa zamani wa FARC waliopinga makubaliano ya mwaka 2016, ambayo yaliwezesha kundi hilo la waasi kusajiliwa kamaa chama cha kisiasa, wanachukuliwa na serikali kama "waasi" hatari kwa nchi. Wanashtumiwa kuua wanaharakati, kufanya biashara ya mihadarati na kushiriki katika shughuli haramu za uchimbaji madini.

Kulingana na vyanzo vya usalama, kuna wapiganaji wapatao 2,500 kati ya waasi hao waliojitenga na FARC, ikiwa ni pamoja na makamanda mashuhuri Ivan Marquez na Jesus Santrich ambao mwanzoni waliunga mkono makubaliano ya amani.