MAREKANI-AFYA

Coronavirus / Marekani: Texas yafuta marufuku ya uvaaji barakoa

Gavana wa jimbo la Texas Greg Abbott awataka maafisa katika jimbo hilo kutowachukulia hatua watu ambao wataonekana hawavai barakoa katika jimbo la Texas.
Gavana wa jimbo la Texas Greg Abbott awataka maafisa katika jimbo hilo kutowachukulia hatua watu ambao wataonekana hawavai barakoa katika jimbo la Texas. AP - Eric Gay

Gavana wa Texas Greg Abbott ametoa agizo linaloondoa marufuku ya uvaaji barakoa na vizuizi vya biashara katika jimbo hilo la Marekani, ikiwa ni ulegezaji mkubwa wa hatua za kiafya hadi sasa katika nchi hiyo, iliyoathiriwa zaidi duniani na janga la Corona.

Matangazo ya kibiashara

Uamuzi wa kuruhusu biashara nyingi za Texas kufunguliwa wiki ijayo unakuja wakati majimbo mengi ya Marekani na miji mikubwa kote nchini imeshuhudia kupungua kwa idadi ya maambukizi mapya ya kila siku na wagonjwa hospitalini.

Kampuni kadhaa, ikiwa ni pamoja na makampuni ya kutengeneza magari, General Motors na Toyota na maduka ya Target na Macy's, wamebaini kwamba  wafanyakazi wao huko Texas wataendelea kuvaa barakoa katika sehemu zao za kazi.

"Sasa ni wakati wa kufungua Texas 100%," amesema gavana wa wa jimbo hilo kutoka chama cha Republican katika mkutano na waandishi wa habari. Amesema agizo hilo litaanza kutumika mnamo Machi 10.

Agizo hilo linafuta marufuku ya uvaaji barakoa katika jimbo la Texas na kuwakataza viongozi wa jimbo hilo kuchwachukulia hatua watu ambao wataonekana hawavai barakoa. Biashara zimeruhusiwa kufunguliwa tena katika jimbo hilo ambapo idadi ya wagonjwa hospitalini imepungua.