BRAZILI

Brazil: Maandamano yaibuka dhidi ya ubaguzi wa rangi

Wanaharakati wa haki za binadamu wameshutumu polisi kwa "mauaji ya kiholela", wakisema vifo vingi havikuchunguzwa.
Wanaharakati wa haki za binadamu wameshutumu polisi kwa "mauaji ya kiholela", wakisema vifo vingi havikuchunguzwa. REUTERS - UESLEI MARCELINO

Raia wa Brazili wameandamana katika miji miwili mikubwa nchini humo kupinga ubaguzi wa rangi, vitendo vinavyotekelezwa na maafisa wa polisi dhidi ya jamii za watu weusi, kulingana na vuguvugula kutoka Marekani la Black Lives Matter, na kumshtumu rais wa nchi hiyo kwa mauaji ya kimbari.

Matangazo ya kibiashara

Miji hiyo ilikumbwa na maandamano makubwa Alhamisi wiki hii, huku polisi ikijaribu kuzuia maandamano hayo kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi, na kuwakamata waandamanaji kadhaa.

Wakati wa jioni, watu elfu moja waliandamana katikati mwa jiji la Rio de Janeiro wakiwa wameshika mishumaa na mabango yalioandikwa "Usiniue, angamiza ubaguzi wa rangi", na kumshtumu Rais wa mrengo wa kulia Jair Bolsonaro kwa mauaji ya kimbari, kupitia vurugu za polisi.

Maneno mengine yaliyoandikwa kwenye mabango hayo yamelaani vifo vya watu 28 waliopigwa risasi katika eneo lenye makazi duni nje kidogo ya mji wa Rio de Janeiro wiki iliyopita wakati wa operesheni ambayo polisi walisema ililenga wauzaji wa madawa ya kulevya.

Wanaharakati wa haki za binadamu wameshutumu polisi kwa "mauaji ya kiholela", wakisema vifo vingi havikuchunguzwa. Jaji wa Mahakama Kuu amesema aliona dalili za watu "walionyongwa kiholela" wakati wa uvamizi katika eneo lenye makazi duni.

Huko Sao Paulo, maelfu ya waandamanaji walikusanyika kupinga ubaguzi wa rangi.