CUBA-VENEZUELA

Rais wa Venezuela atangaza uungwaji wake mkono kwa raia na serikali ya Cuba

Watu wanaendelea kuandamana dhidi ya serikali ya Miguel Diaz-Canel, huko Havana, Julai 11, 2021.
Watu wanaendelea kuandamana dhidi ya serikali ya Miguel Diaz-Canel, huko Havana, Julai 11, 2021. © YAMIL LAGE / AFP

Rais wa Venezuela Nicolas Maduro, mshirika mkubwa wa Havana, ameweka wazi msimamo wake kwa yale yanayoendelea nchini Cua, akibaini kwamba anaunga mkono mwenzake Miguel Diaz-Canel, "raia wa Cuba" na "kwa serikali ya mapinduzi ya Cuba", siku moja baada ya maandamano ya kupinga serikali.

Matangazo ya kibiashara

Nicolas Maduro amesema "Venezuela na Cuba ni nchi rafiki tena ndugu wa karibu, na kusema kuwa bila shaka Cuba itaondokana na shida inazopitia kwa sasa”.

Awali Rais wa Cuba Miguel Diaz-Canel alilaaani vikwazo vya Marekani, ambavyo vimeongezwa katika miaka ya hivi karibuni, shida za kiuchumi ambazo nchi inakabiliwa nazo, hasa na uhaba wa dawa na kukata mara kwa mara kwa umeme, kutokana na maandamano ambayo hayajawahi kutokea kwa miongo kadhaa mwishoni mwa wiki hii iliyopita.

Akiongea kwenye televisheni, huku akizungukwa na wajumbe wa serikali yake, kiongozi huyo wa Cuba amesema ukosoaji dhidi ya udhibiti wa janga la COVID-19 nchini Cuba unalenga kuvunja umoja wa wananchi wa taifa hilo.Miguel Diaz-Canel amelaani matukio ya vurugu na uporaji ambao ulifanyika katika miji kadhaa ya nchi, akishtumu tabia hiyo "mbaya kabisa ya waandamanaji, isiyo ya adabu na ya kihuni".

Rais wa Marekani Joe Biden, kwa upande wake, aliwahakikishia raia wa Cuba kuwa Marekani inawaunga mkono mbele ya kile alichoonyesha kama miongo kadhaa ya ukandamizaji na usimamizi usiofaa kabisa wa mgogoro wa kiafya unaosababishwa na janga la COVID-19.

"Raia wa Cuba kwa ujasiri wanadai haki za kimsingi zinazokubalika kimataifa. Haki hizi, pamoja na haki ya kuandamana kwa amani na haki ya kuchagua kwa uhuru mustakabali wa nchi yao, lazima ziheshimiwe," alisema katika taarifa.

Marekani inatoa wito kwa utawala wa Cuba kuwasikiliza raia wake na kukidhi mahitaji yao kwa wakati huu muhimu kuliko kujitajirisha.