HAITI-USALAMA

Rais wa Haiti Jovenel Moïse azikwa Cap Haitien

Maafisa wakiaga mwili wa Jovenel Moise.
Maafisa wakiaga mwili wa Jovenel Moise. REUTERS - RICARDO ARDUENGO

Wananchi wa Haiti wamemzika rais wao Jovenel Moïse aliyeuawa nyumbani kwake baada ya kundi la watu wenye silaha kuvamia makazi yake binafsi huko Port-au-Prince wiki tatu zilizopita.

Matangazo ya kibiashara

Polisi ya Haiti inawashikilia karibu watu 20, ikiwa ni pamoja na wanajeshi kadhaa wa zamani wa Colombia wanaotuhumiwa kuwa sehemu ya kundi la watu waliokuja kumuua Jovenel Moïse, lakini bado uchunguzi unaendelea.

Polisi ya Colombia, ambayo pia inafanya uchunguzi kuhusiana na mauaji hayo, siku ya Ijumaa ilisema kwamba afisa wa zamani wa wizara ya sheria ya Haiti, Joseph Felix Badio, aliamuru mamluki wawili wa Colombia wamwue rais Jovenel Moïse.

Vurugu zazuka kabla ya mazishi

Kulishuhudiwa machafuko Alhamisi wiki hii katika mji wa kaskazini nchini Haiti, wa Cap-Haitien wakati waandamanaji walipoweka vizuizi barabarani wakipinga mauaji ya Rais Jovenel. Polisi waliokwenda kwenye mji huo kwa ajili ya kusaidia kusimamia mazishi ya rais huyo walikutana na waandamanaji ambao ni wafuasi wa kiongozi huyo wanaowataja polisi kuhusika na mauaji kwenye makazi ya rais Julai 7. Mtu mmoja amekufa kwenye vurugu hizo.

Aidha Marekani imemtangaza Daniel Foote kuwa mjumbe maalumu atakayesaidia kuratibu misaada ya Marekani nchini Haiti pamoja na juhudi za kupatikana amani ya kudumu na uchaguzi baada ya mauaji hayo ya Rais Moise.

Haiti chini ya utawala wa Jovenel Moise

Taifa hilo lenye wakaazi milioni 11 limezidi kukosa utulivu na kuwa lenye chuki chini ya utawala wa Moise. Madhila yake ya kiuchiúmi, kisiasa na kijamii yameongezeka huku vurugu za magenge zikishika kasi hasa katika mji mkuu Port-au-Prince.

Mfumuko wa bei umeongezeka pakubwa katika taifa ambako asilimia 60 ya wakaazi wanapata chini ya dola mbili kwa siku. Moise aliekuwa na umri wa miaka 53, amekuwa akitawala kwa amri ya rais kwa zaidi ya miaka miwili, baada ya nchi hiyo kushindwa kufanya uchaguzi, hatua iliyopelekea kuvunjwa bunge.