Rais Joe Biden awatuliza nyoyo raia kutokuwa na wasiwasi kuhusu kirusi kipya cha Omicron

Rais wa Marekani Joe Biden, amesema kirusi kipya cha Covid 19 kilichopewa jina la Omicron, kinazua mashaka, lakini watu hawapaswi kuwa na hofu.

Rais Joe Biden wakati wa mkutano na viongozi wa kampuni, katika maktaba ya Eisenhower Executive Office Building, White House, Jumatatu, Novemba 29, 2021 huko Washington.
Rais Joe Biden wakati wa mkutano na viongozi wa kampuni, katika maktaba ya Eisenhower Executive Office Building, White House, Jumatatu, Novemba 29, 2021 huko Washington. © AP Photo/Evan Vucci
Matangazo ya kibiashara

Kauli ya Biden imekuja, siku moja baada ya kirusi hicho kugundulika, nchini Canada na kuwataka Wamarekani kuendelea kupokea chanjo.

 

Mataifa mbalimbali duniani, ikiwemo Marekani na yale ya Umoja wa Ulaya yamesitisha safari za ndege kutoka mataifa ya Kusini mwa Afrika, baada ya kirusi hicho kugundulika nchini Afrika Kusini wiki iliyopita.

Hayo yanajiri wakati shirika la Afya Duniani, WHO, linaonya juu ya 'hatari kubwa ya kuambukizwa' kote ulimwenguni, kufuatia kuzuka kwa aina mpya ya kirusi cha Corona cha Omicron.

Mkuu wa shirika hilo, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus, alitoa wito upya wa kushinikiza jamii ya kimataifa kutoa chanjo kwa mataifa maskini.  

Visa tayari vimeripotiwa katika nchi kadhaa zikiwemo Canada, Uingereza, Ureno, Ubelgiji na Uholanzi.

Omicron imesababisha Uingereza, EU na Marekani kutoa marufuku ya kusafiri kwa nchi za Kusini mwa Afrika - uamuzi ulioshutumiwa na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa.