PAKISTAN

Hillary Clinton afanya ziara ya kushitukiza Pakistan

RFI

Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Marekani, Hillary Clinton amefanya ziara ya kushitukiza nchini Pakistan akiwa na lengo la kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili unaoonekana kuyumba katika siku za hivi karibuni kufuatia kuuawa kwa kwa aliyekuwa kiongozi wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda Osama Bin Laden.Bi. Clinton anakuwa kiongozi wa pili wa ngazi za juu nchini Marekani kutembelea Pakistan baada ya kifo cha Osama na ziara hiyo imezua gumzo na watu wakitaka kujua nini kitatokea. 

Matangazo ya kibiashara

Ziara hiyo imekuja siku chache baada ya Jeshi la Marekani kutangaza kuwa litaendelea kupunguza idadi wanajeshi wake walioko nchini Pakistan baada ya kupokea ombi la Serikali ya Pakistan la kuitaka Marekani kuanza kupunguza uwepo wa wanajeshi wake hali ambayo imeibua maswali mengi kuhusu uhusiano wa nchi hizo mbili. 

Wizara ya Mambo ya ndani nchini Marekani ilisema kuwa imeamua kutekeleza uamuzi wa kupunguza wanajeshi wake ili kukidhi matakwa ya Serikali ya Pakistan.

Ombi hilo Pakistan linakuja baada ya jeshi maalum la Marekani Kumuua alikuwa kiongozi wa kundi la kigaidi la Al- Qaeda, Osama Bin Laden aliyekuwa amejificha nchini humo mapema mwezi Mei mwaka huu.

Marekani pamoja na wanajeshi wengine ina askari takriban 200 ambao wako nchini Pakistan wakitoa mafunzo ya kijeshi lakini wamekuwa wakidaiwa kuwa wanafanya shughuli za kiintelijinsia nchini humo.

Ombi hilo la Pakistan kwa Marekani limeibua gumzo kuwa huenda Pakistan inaanza kukata uhusiano na Marekani kutokana na kutofurahishwa kwake na tuhuma kuwa ilitambua taarifa za Osama kujificha nchini humo.