CHINA

Mwanaharakati nchini China Ai Weiwei aachiwa huru kwa dhamana

msanii mwanaharakati wa China Ai Weiwei
msanii mwanaharakati wa China Ai Weiwei AFP/Peter Park

Hatimaye, msanii na mwanaharakati maarufu nchini Uchina, Ai Weiwei ametolewa nje kwa dhamana na amesema ana furaha kubwa kurudi nyumbani, baada ya kushikiliwa na polisi tangu mwezi wa nne, mwaka huu.

Matangazo ya kibiashara

Shirika la habari la Shinhua limesema Weiwei, mwenye umri wa miaka hamsini na minne ameachiwa, baada ya kukiri kukwepa kulipa kodi na ukweli kwamba anakabiliwa na ugonjwa wa kisukari.

Na Shirika la habari la Ufaransa AFP, lilipomuuliza juu ya hali yake, Weiwei akajibu tu kwamba, hawezi kutoa maelezo zaidi kwani yuko nje kwa dhamana ila amefurahi kuungana tena na familia yake.

Akiwa katika uwanja wa ndege wa Hong Kong, tarehe tatu mwezi April, polisi walimkamata Weiwei, tukio lililolaaniwa na mataifa mengi pamoja na mashirika ya kutetea haki za binadamu.

Polisi wanadai kuwa Weiwei ameachiwa kutokana na tabia yake njema ya kukiri makosa yake, utayari wake wa kulipa kodi anazodaiwa pia kutokana na ugonjwa unaomkabili.