Thailand

Jeshi la Thailand lakubali ushindi wa chama cha upinzani

Wananchi wa Thailand wakipanga foleni kwa kupiga kura  Juni 03/07/2011
Wananchi wa Thailand wakipanga foleni kwa kupiga kura Juni 03/07/2011 REUTERS

Jeshi nchini Thailand, limekubali ushindi wa chama cha upinzani, likisema wazi kuwa raia wa taifa hilo wameamua hivyo, kilichobaki ni kukubali matokeo na kujenga nchi. 

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa ulinzi ambaye anamaliza muda wake, Jenerali Prawit Wongsuwon, ametoa tamko hilo baada ya kufanya kikao na viongozi wa juu wa jeshi hilo lenye nguvu nchini Thailand, na wamemhakikishia kuwa jeshi litakiruhusu chama cha Peu Thai, kuongoza nchi.

Kitendo hicho, kimeleta matumaini nchini humo na kuondoa hofu ya kutokea kwa mapinduzi.

Haya yanajiri, baada ya tume ya uchaguzi kutangaza kuwa upinzani, ambacho ni chama cha kiongozi wa zamani Thaksin Shinawatra, kimepata viti 265, kati ya nafasi 500 za wabunge.

Chama cha waziri mkuu anayeondoka Abhisit Vejjajiva, Democrats, ambaye amekubali matokeo hayo, kimeambulia viti 159 pekee.

Asilimia 75 kati ya wapiga kura waliojiandikisha kushiriki katika uchaguzi, walijitokeza kutumia haki yao ya msingi, idadi ambayo ni sawa na iliyoshuhudiwa mwaka 2007.