Yemen

Afisa mkuu wa intelijensia mjini Aden auawa na watu wenye silaha

Maandamano makubwa ya kumtaka rais Ali Abdallah Saleh aachie ngazi  Julay 17, 2011.
Maandamano makubwa ya kumtaka rais Ali Abdallah Saleh aachie ngazi Julay 17, 2011. REUTERS/Khaled Abdullah

Afisa mkuu wa intelijensia wa mjini Aden ameuawa na watu wenye silaha tukio jipya la mauaji kulikumba eneo hilo la kusini mwa Yemen.

Matangazo ya kibiashara

Luteni kanali Ali Ahmed Abd Rabo alikuwa akiendesha gari kandokando ya barabara ya pwani jana jioni na baadae kuzuiliwa na waandamanaji. Watu wenye silaha walilifyatulia risasi gari hilo shambulio lililosababisha Rabo kupoteza maisha.

Haijatambuliwa ni nani alihusika katika mauaji hayo ns haijatanabaishwa ikiwa wauaji hao walitoka katika kundi la waandamanaji ama wanamgambo waliojipenyeza katikati ya waandamanaji. Magharibi mwa mji wa Aden ,mkuu wa majeshi kanali Naji Aitha alinusurika kifo baada ya wanamgambo kulipua mabomu nje ya makazi yake jana.

wakati hayo yakiendelea Rais wa Yemen Ali Abdullah Saleh amemuidhinisha makamu wake kujadiliana na upinzani juu ya maswala yahusuyo mabadiliko ya kisiasa, hatua inayoonesha kuwa kiongozi huyo hatimaye ameridhia pendekezo ya jumuia ya nchi za ghuba la kumaliza mgogoro wa kisiasa uliodumu miezi kadhaa.

Saleh aliyekuwa nje ya Yemen kwa zaidi ya miezi mitatu amemkabidhi makamu wa rais Abdrabuh Mansur Hadi mamlaka kufanya mazungumzo na upinzani juu ya namna ya kufanya mabadiliko ya kisiasa nchini humo.

Saleh aliyetawala Yemen tangu mwaka 1978 yuko nchini Saudi Arabia akitazama afya yake baada ya shambulio la bomu la juni 3 katika makazi yake amemtaka makamu huyo wa Rais kuanza mchakato wa maandalizi ya uchaguzi wa urais utakaosimamiwa na waangalizi wa ndani na wale wa nje.