INDIA

Watu zaidi ya 100 wapoteza maisha baada ya kunywa pombe yenye sumu

Watu mia moja na mbili wamethibitishwa kupoteza maisha Mashariki mwa India baada ya kunywa pombe yenye sumu duru za kitabubi zimethibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Matangazo ya kibiashara

Tukio hilo limetokea katika Wilaya ya 24-Parganas ambapo Mkuu wa Wilaya hiyo Narayan Swarup amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo baada ya watu hao kunywa pombe ya kienyeji.

Taarifa za awali kutoka katika hospital waliyofikishwa marehemu hao zinasema kuwa wamebaini watu hao walikunywa pombe ya kienyeji ambayo ilikuwa imewekwa sumu ya methanol.

Methanol hiyo imebaini kwa waathirika wengine ishirini ambao wamebahatika kupona licha ya hali zao kutokuwa nzuri na kwa sasa wanaendelea kupatiwa matibabu ikiwemo ni pamoja na kuondoa sumu iliyopo mwilini.

Mkuu wa Polisi katika eneo hilo Chiranjib Murmu amesema taarifa za awali za kitabibu zinathibitisha vifo hivyo kuchangiwa na sumu ya methanol lakini kwa sasa wameanza uchunguzi ambao utasaidia kubaini nani ambaye aliweka sumu hiyo.

Pombe hiyo ya kienyeji imekuwa ikinywewa sana na watu wenye kipato cha chini nchini India wakiwemo madereva na hata wafanyakazi ambao wanafanya vibarua ili kuweza kujikimu kwa maisha yao.

Pombe hiyo imekuwa ikiuzwa kwa rupee sita kwa lita moja sawa kabisa na dola senti kumi na moja kitu ambacho kimekuwa ni rahisi kwa wananchi wa kipato cha chini kuweza kumudu gharama zake.

Vifo vinavyosababishwa na unywaji wa pombe yenye sumu nchini India imekuwa ni hali ya kawaida kwani wananchi wengi wamekuwa wanywaji wa pombe za kienyeji ambazo utengenezaji wake haufuati taratibu za kitaaluma.