PHILIPPINES

Watu zaidi ya 650 wahofiwa kupoteza maisha nchini Ufilipino kutokana na mafuriko

Waokoaji nchini Philippines wakijaribu kuwaokoa wananchi walionaswa kwenye mafuriko
Waokoaji nchini Philippines wakijaribu kuwaokoa wananchi walionaswa kwenye mafuriko Reuters

Serikali nchini Ufilipino imetangaza kuanza operesheni kubwa ya uokoaji kusini mwa nchi hiyo katika juhudi za kuwanusuru maelfu ya wananchi waliokumbwa na mafuriko. 

Matangazo ya kibiashara

Zaidi ya wa 650 wanahofiwa kupoteza maisha katika mji wa Cagayan De Oro kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini humo na kusababisha maafa makubwa kwa wananchi wanaoishi maeneo ya mabondeni.

Katika hatua nyingine kitengo cha maafa nchini humo kimetangaza kuwa watu zaidi ya 808 katika mji huo hawajulikani walipo mpaka sasa lakini juhudi za kuwatafuta zinaendelea.

Hata hivyo wakati Serikali ikiongeza nguvu zaidi za uokojai ikiwa ni pamoja na kuomba msaada toka jumuiya ya kimataifa, bado juhudi hizo zimekuwa ngumu kutokana na maeneo mengi ya mji huo miundo mbinu yake kuharibika ikiwemo ukosefu wa nishati ya umeme.

Mmoja wa maofisa wa Serikali ya Ufilipino amesema kuwa licha ya wanajeshi wengi kupelekwa katika maeneo ambayo yameathirika lakini juhudi zao zimekwamishwa kutokana na barabara nyingi kuharibiwa vibaya na hivyo kushindwa kufika kwa wakati katika maeneo mengi.

Mamlaka ya hali ya hewa imetangaza kuendelea kunyesha kwa mvua hizo huku mji wa Mindanao ukielezwa kuwa utaathirika zaidi na mvua hizo ambazo zimeambatana na upepo mkali.

Watu zaidi ya laki moja wanaelezwa kuyakimbia makazi yao kutokana na mvua hizo huku mpaka sasa ikielezwa zaidi ya nyumba elfu kumi zimeharibiwa.