PAPUA NEW GUINEA

Serikali ya Papua New Guinea yatangaza kuwasamehe wanajeshi watakaosalimisha silaha zao

Wanajeshi walioasi na kutaka kuipindua serikali ya Papua News Guinea juma lililopita
Wanajeshi walioasi na kutaka kuipindua serikali ya Papua News Guinea juma lililopita Reuters

Serikali ya Papua New Guinea imetangaza kuwaachia huru wanajeshi wote walioshiriki katika jaribio la kufanya mapinduzi juma lililopita endapo wanajeshi hao watasalimisha silaha zao.

Matangazo ya kibiashara

Naibu waziri mkuu Belden Namah amesema kuwa serikali itawasamehe wanajeshi wote ambao bado wanaendelea kushikilia silaha walizozitumia wakati wa jaribio la kutaka kuipindua serikali.

Akizungumza kupitia njia ya televisheni, naibu waziri mkuu huyo amesema kuwa endapo wanajeshi hao watajisalimisha kwa hiari yao basi hawatochukuliwa hatua na kuonya endapo wataruida tena serikali haitavumilia.

Zaidi ya wanajeshi mia mbili walioasi walijikusanya katika uwanja wa Taurama wakiwa na silaha tayari kuweza kuzisalimisha kwa serikali ingawa taarifa hizo hazijathibitihshwa rasmi kama ni kweli walikuwa wakitaka kufanya hivyo.

Naibu waziri mkuu huyo amesema kuwa serikali pekee inayotambuliwa nchini humo ni ya waziri mkuu O'Neill-Namah na sio serikali nyingine yoyote ambayo itapatikana kwa njia zisizo halali.

Nchi ya Papua New Guinea imekuwa katika mgogoro wa kisiasa toka kurejea kwa waziri mkuu wa zamani Michael Somare ambaye anadai ndie kiongozi halali wa nchi hiyo.