MYANMAR

Aung San Suu Kyi pamoja na wabunge wengine 33 wa NLD wala kiapo kuwa Wabunge nchini Myanmar

Kiongozi wa Upinzani Nchini Myanmar Aung San Suu Kyi akila kiapo pamoja na wabunge wengine 33 katika Bunge la nchi hiyo huko Naypyiadaw
Kiongozi wa Upinzani Nchini Myanmar Aung San Suu Kyi akila kiapo pamoja na wabunge wengine 33 katika Bunge la nchi hiyo huko Naypyiadaw

Kiongozi Mkuu wa Upinzani nchini Myanmar na Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Aung San Suu Kyi hatimaye amekula kiapo cha kuwa Mbunge wa Bunge la nchi hiyo pamoja na wabunge wengine thelathini na watatu kutoka Chama chake cha NLD.

Matangazo ya kibiashara

Suu Kyi ameandika historia mpya ya kuanza harakati zake za kuhakikisha anafanikisha kusimika demokrasia katika nchi hiyo ambayo kwa karibu miongo miwili ilikuwa chini ya utawala wa Kijeshi ambao unashutumiwa vikali kwa kubinya uhuru wa demokrasia.

Kiongozi huyo wa Chama cha NLD mwenye umri wa miaka 66 kwa sasa ameapishwa katika shughuli ambayo imefanyika katika Bunge la nchi hiyo lililopo katika Mji Mkuu Naypyidaw hatua ambayo inaashiria kuanza kwa shughuli zake rasmi akiwa Mbunge.

Hatua hii ya kula kiapo kwa Suu Kyi inakuja baada ya Kiongozi huyo wa Chama Cha NLD kuwa katika kifungo cha ndani kwa mia ishirini kutokana na kuwa mstari wa mbele kukosoa utawala wa kijeshi.

Suu Kyi aligomea kula kiapo juma lililopita akitaka mabadiliko kwenye kiapo hicho hasa sehemu ambayo inamtaka Mbunge aseme atailinda serikali ya Kijeshi kitendo ambacho yeye anaamini kitakuwa kinambana kufanya shughuli zake za kimapinduzi.

Mshindi huyo wa Tuzo ya Amani ya Nobel baada ya kula kiapo hicho amesema amefikia hatua ya kula kiapo kuhakikisha anapigania haki za wananchi ikiwa ni pamoja na kufanyika kwa mabadiliko ya katiba iwe ya kiraia.

Uamuzi wa Suu Kyi kula kiapo aliutoa siku ya jumatatu ikiwa ni siku moja kabla ya kukutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki Moon ambaye alifanya ziara nchini Myanmar ikiwa ni hatua ya kuangalia mafanikio ambayo yamefikiwa.

Katibu Mkuu wa UN Ban akiwa ziarani nchini Myanmar aliweka bayana mafanikio ambayo yamepatikana na kuzitaka nchi za Magharibi kuondoa vikwazo ili kuipa nafasi nchi hiyo iweze kupiga hatua za kimaendeleo.