MYANMAR-THAILAND

Kiongozi wa Upinzani Nchini Myanmar Suu Kyi kufanya ziara ya kwanza nje ya nchi baada ya miaka 24

Kiongozi wa Upinzani Nchini Myanmar na Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Aung San Suu Kyi anayetarajia kuzuru Thailand hii leo
Kiongozi wa Upinzani Nchini Myanmar na Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Aung San Suu Kyi anayetarajia kuzuru Thailand hii leo REUTERS/Damir Sagolj

Kiongozi Mkuu wa Upinzani nchini Myanmar na Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Aung San Suu Kyi anafanya ziara ya kwanza nje ya nchi hiyo katika kipindi cha miaka ishirini na minne ambayo alikuwa anakutana na mbinyo wa kisiasa kutoka kwa Utawala wa Kijeshi uliokuwa unatawala.

Matangazo ya kibiashara

Ziara hii ya kwanza ya Suu Kyi anaifanya nchini Thailand kuhudhuria Kongamano la Kiuchumi la Dunia linalozileta pamoja nchini za Asia Mashariki ambapo Mynamar ni miongoni mwa nchi zitakazoudhuria kuangalia suala la uchumi.

Mfungwa huyo wa zamani wa nyumbani ambaye alifanikiwa kushinda ubunge mwezi April akiwa kwenye Kongamano hilo la Kiuchumi kando atakutana na Waziri Mkuu wa Thailand Yingluck Shinawatra.

Katibu Mkuu wa Waziri Mkuu wa Thailand Shinawatra, Thawat Boonfeung amethibitisha kufanyika kwa mkutano huo lakini ameshindwa kusema muda ambao utafanyika kwani hadi sasa ratiba hainaweka bayana.

Suu Kyi awali alikuwa anahofia kama angepata ruhusa ya serikali kwenda kuhudhuria Kongamano hilo lakini baadaye akapata uhakika wa kuruhusiwa kwenda na itakuwa mara ya kwanza tangu mwaka 1988.

Serikali kupitia Ofisa wake mmoja amesema wamemruhusu Suu Kyi kwenda kwenye Kongamano hilo lakini pia kurejea nyumbani ambako atafanya shughuli zake za kisiasa bila ya kukumbana na kipingamizi cha aina yoyote.

Ziara hii ni mwanza wa mfululizo wa ziara za Suu Kyi ambaye amezipanga kuzifanya katika Mataifa ya Ulaya ikiwemo Denmark, Uswiss na kisha Uingereza ikiwa ni sehemu ya kuonesha kuheshimiwa kwa demokrasia kunakofanywa na serikali mpya.

Marekani, Uingereza na Umoja wa Ulaya EU kwa pamoja wametangaza kulegeza vikwazo kwa nchi ya Myanmar baada ya kuonekana kuanza kuheshimu haki za binadamu na kutoa uhuru kwa demokrasia kuchukua mkondo wake.