India

Washukiwa watano wa ubakaji nchini India kufikishwa mahakamani leo

Raia nchini India wakishinikiza kutolewa kwa adhabu kali dhidi ya Wabakaji
Raia nchini India wakishinikiza kutolewa kwa adhabu kali dhidi ya Wabakaji REUTERS/Amit Dave/File

Wanaume watano wanaoshutumiwa kuhusika na kitendo cha ubakaji dhidi ya mwanafunzi wa miaka 23 mjini New Delhi wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza hii leo huku kukiwa na wito wa Raia nchini India kutaka watu hao wanaoshutumiwa kunyongwa.

Matangazo ya kibiashara

Watano hao ambao watakutwa na adhabu ya kifo iwapo watakutwa na hatia , wanashutumiwa kujihusisha na ubakaji na unyang'anyi katika tukio la tarehe 16 mwezi Desemba mwaka jana tukio lililosababisha Raia nchini humo kufanya maandamano kupinga unyanyasaji dhidi ya Wanawake.
 

Mgomo wa Wanasheria kadhaa kupinga mawakili waliokuwa mstari wa mbele kuwatetea washtakiwa, ulisababisha kucheleweshwa kuanza kwa kesi mahakamani hapo ambapo askari walilazimika kutuliza ghasia hizo.
 

Kwa kawaida huchukua miezi kwa ofisi ya mwendesha mashtaka kufungua Kesi, lakini hali ni tofauti kwa kesi hii ambayo kesi imefunguliwa takriban juma moja baada ya kifo cha Binti huyo aliyepoteza maisha nchini Singapore kufuatia majeraha aliyoyapata.
 

Polisi wwameweka ulinzi mkali wakati huu kesi inaposikilizwa kwa ajili ya kulinda usalama wa washukiwa.Mtu mmoja alikamatwa juma lililopita akishutumiwa kujaribu kutega bomu karibu na makazi ya Mshukiwa mmoja.