KOREA KUSINI

Waziri Mkuu wa Korea Kusini atembelea kisiwa cha Yeonpyeong

Waziri Mkuu wa Korea Kusini Chung Hong-won ametembelea kisiwa cha Yeonpyeong ambacho Korea Kaskazini inakitaja kama moja ya maeneo ambayo huenda ikayavamia. Akiwa katika eneo hilo Hong-won ametoa wito kwa wananchi kuwa watulivu na kuvisihi vikosi vya kijeshi kuwa tayari kukabiliana na maadui endapo kutakuwa na tishio lolote la usalama.

english.yonhapnews.co.kr
Matangazo ya kibiashara

Ziara hiyo inakuja siku kadhaa baada ya kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-Un kuzuru katika eneo la mpaka na kuionya jirani yake Korea Kusini kuwa itafanya mashambulizi katika kisiwa kingine chenye mgogoro cha Baengnyeong.

Katika siku za hivi karibuni vyombo vya habari vya Korea Kaskazini vimeripoti ziara kadhaa za kiongozi wa Taifa hilo katika vikosi vya kijeshi katika eneo la mpaka wa mataifa hayo mawili yenye uhasama.

Visiwa vya Korea Kusini karibu na mpaka vimekuwa vikionekana kama kitovu cha mgogoro kati ya mataifa hayo mawili huku serikali ya Pyongyang ikitishia kuvamia hali inayosababisha hofu ya usalama kwa wakazi wa maeneo hayo.

Kumekuwepo na taarifa za wanajeshi wa Marekani na wale wa Korea Kusini kuanza kuyafanya mazoezi ya pamoja na kujiweka tayari kwa mashambulizi kutoka Pyongyang.