PAKISTAN

Wafuasi wa Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan Nawaz Sharif waanza kusherekea ushindi wa matokeo ya awali

Wafuasi wa Muslim League (PML-N) chini ya uongozi wa Waziri mkuu wa zamani wa Pakistan Nawaz Sharif wameanza kusherekea ushindi katika mitaa mbalimbali ya nchi hiyo baada ya matokeo ya awali ya kura zilizopigwa jumamosi nchini humo kuonyesha chama hicho kinaongoza kwa asilimia kubwa katika kujinyakulia viti vingi vya ubunge.

REUTERS/Mohsin Raza
Matangazo ya kibiashara

Matokeo rasmi ya uchaguzi huo bado hayatangazwa lakini takwimu zisizo rasmi zimebainisha kuwa Muslim League wamepata zaidi ya viti 100 kati ya 272 vya bunge la nchi hiyo.

Ushindi wa Muslim League umechangiwa pakubwa na jimbo la Punjab ambalo ni maskani ya Sharif lenye takribani asilimia 60 ya wapiga kura wote wa Pakistan, hata hivyo atatakiwa kupata uungwaji mkono kutoka katika majimbo matatu madogo ili kukamilisha ushindi huo.

Chama cha Movement of Justice (PTI) kinachoongozwa na mcheza kriketi wa zamani Imran Khan kimefanya vizuri katika jimbo la Peshawar kikiwa katika nafasi ya pili sambamba na Chama cha Pakistan Peoples Party (PPP) cha Rais wa nchi hiyo Asif Ali Zardar ambao hata hivyo huenda kwa pamoja wakanyakua viti chini ya arobaini vya ubunge.

Chama cha Waziri Mkuu anayemaliza muda wake Raja Pervez Ashraf kimeanguka vibaya katika uchaguzi huo.

Wapiga kura walijitokeza kwa wingi licha ya vitisho vilivyotolewa na kundi la Taliban, kumeripotiwa kutokea mashambulizi mbalimbali ambapo polisi wamethibitisha kuuawa kwa watu 11 na wengine zaidi ya 40 kujeruhiwa katika mlipuko wa bomu mjini Karachi siku ya jumamosi.