PAKISTANI

Nawaz Sharif aanza mazungumzo ya kuunda serikali mpya ya Pakistan

AFP PHOTO / ARIF ALI

Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan Nawaz Sharif ambaye Chama chake kimefanikiwa kupata viti vingi katika Bunge la nchi hiyo ameanza mazungumzo na vyama vingine vya siasa kuhakikisha anaunda serikali mpya baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa siku ya jumamosi. Chama cha Kiislam cha PML-N anachotoka Sharif kimefanikiwa kupata ushindi huo wa kishindo lakini hakina uwezo wa kuunda serikali peke yake hivyo kinahitaji kuungwa mkono.

Matangazo ya kibiashara

Sharif anakuwa Waziri Mkuu wa Pakistan kwa mara ya tatu, muhula wake wa mwisho ulikomeshwa miaka 14 iliyopita baada ya kufanyika mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani kabla ya kufungwa na baadaye kuishi uhamishoni Saudi Arabia mpaka mwaka 2007 aliporejea nchini humo.

Ushindi wa chama cha Sharif umechangiwa na idadi kubwa ya wapiga kura katika jimbo lake la Punjab ambalo lina takribani asilimia 60 ya wapiga kura wote wa Pakistan.

Mchezaji wa zamani wa Kriketi na Mpizani mkubwa wa Sharif, Imran Khan akiwa Hospital amekubali matokeo hayo na amesema Chama chake kinajiandaa kuwa wapinzani licha ya kukiri amesikitishwa na taarifa za uwepo wa wizi wa kura.

Katika uchaguzi huo uliofanyika siku ya jumamosi wapiga kura walijitokeza kwa wingi licha ya vitisho vilivyotolewa na kundi la Taliban, mashambulizi mbalimbali yaliripotiwa ambapo watu 11 waliuawa na wengine zaidi ya 40 kujeruhiwa katika mlipuko wa bomu mjini Karachi.