INDIA

Kiongozi wa kundi la kigaidi la Indian Mujahideen Yasin Bhatkal akamatwa

Polisi nchini India wanasema wamemkamata kiongozi wa kundi la wanamgambo la Indian Mujahideen Yasin Bhatkal,  ambaye amekuwa akituhumiwa kuongoza mashambulizi ya mabomu nchini humo na kusababisha vifo vya mamia ya watu.

Matangazo ya kibiashara

Bhatkal alikamatwa karibu na mpaka wa Nepal na kwa sasa anazuiliwa katika jimbo la Bihar kwa mujibu wa maelezo ya Waziri wa Mambo ya ndani nchini humo Ushilkumar Shinde.

Kundi hilo la Indian Mujahideen lilifahamika mwaka 2007 baada ya kubainika kutekeleza mashambulizi kadhaa katika jimbo la Uttar Pradesh na pia katika miji ya Mumbai, Bangalore, New Delhi na Pune.

Wachambuzi wa maswala ya kigaidi na usalama wanasema kuwa mashambulizi ya kundi hili katika miaka ya hivi karibuni yanaonesha kuwa yanashirikiana na makundi mengine ya kiislamu kama yale ya  Lashkar-e-Taiba na Jaish-e-Mohammed kutoka Pakistan.

Kukamatwa kwa Bhatkal, ambaye wakati mmoja alinaswa na Camera za siri akitegesha bomu mjini Mumbai kunaelezwa na wachambuzi wa usalama kuwa ni ishara kuwa vyombo vya usalama nchini India vimepiga hatua ya kuwasaka viongozi wa kigaidi baada ya mwezi uliopita kumkamata gaidi mwingine Abdul Karim Tunda.

Shambulizi la bomu la hivi karibuni linaloshukiwa kutekelezwa na kundi la Indian Mujahideen lilikuwa mwezi Februari mwaka huu katika mji wa Hyderabad, na kusabisha vifo vya watu 16.

Kundi hili ambalo lina mizizi yake nchini Pakistan linaungwa mkono na Waislamu wenye asili ya Kashmir ambao wanaipinga serikali ya India.