BANGLADESH-Maandamano

Maandamano ya kupinga uchaguzi yaliyoitishwa na upinzani yaendelea nchini Bangladesh

Waziri Mkuu wa Bangladesh Sheikh Hasina amesisistiza kuwa ushindi wa chama chake katika uchaguzi mkuu nchini humo ulikuwa halali licha ya kususiwa na upinzani. Aidha, Hasina amesema hawezi kuzungumza na upinzani na badala yake ameushtumu kwa kusabisha machafuko nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Ushiindi wa Hasina una maana kuwa ataendelea kuongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, ushindi, ambao upinzani unasema si halali na uchaguzi huo haukuwa huru na haki.

Awali, Sheikh Hasina kiongozi wa serikali alisema upinzani umekosea kususia uchaguzi uliokipa chama chake cha Jumuiya ya Awami ushindi wa asilimia 80 ya kura kufuatia kukosekana kwa upinzani katika uchaguzi ambao umegubikwa na ghasia zilizo gharimu maisha ya watu 26.

Chama kikuu cha upinzani cha BNP kilikuwa kinataka kuwepo kwanza na serikali isioegemea upande wowote kabla ya kuelekea kwenye uchaguzi huo, jambo ambalo serikali ilitupilia mbali.

Akizungumza kwa mara ya kwanza baada ya uchaguzi huo, Sheikh Hasina amesema kususia kwa upinzani kwenye uchaguzi huo hakumaanishi kuwa uchaguzi hauna uhalali wowote hasa kwamba wananchi wengi wameshiriki.

Kiongozi huyo amebaini kwamba kabla ya uchaguzi huo alipendekeza kwa mpinzani wake mkuu Khaleda Zia kushiriki katika serikali ya mpito huku wizara kadhaa zikitolewa kwa upinzani kwa ajili ya kuliongoza taifa, mapendekezo ambayo amesema hayakupokelewa.

Sheikh Hasina amesema iwapo upinzani unaokuwa umefanya kosa kubwa sana la kutoshiriki kwenye uchaguzi, hii ni fursa kwao kuonyesha nia ya kuachana na ugaidi na kuleta mapendekezo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ametoa wito kwa uongozi wa chama tawala cha Awami na upinzani kuzungumza ili kumaliza hali ya wasiwasi ya kisiasa nchini humo.