UKRAINE-URUSI-Usalama-Siasa

Mashariki mwa Ukraine: Washington yainyooshea Urusi kidole cha lawama

Waasi wa Ukraine wanaungwa mkono na Urusi wameimarisha ngome zao na kuzidisha mashambulizi dhidi ya jeshi la Ukraine ambalo limekua likiendesha mapigano ili kuiweka kwenye himaya yake miji ya Donetsk na Lougansk.

Rais wa Urusi, Vladimir Putin akiwa Minsk, Agosti 26 mwaka 2014.
Rais wa Urusi, Vladimir Putin akiwa Minsk, Agosti 26 mwaka 2014. REUTERS/Alexei Druzhinin/RIA Novosti/Kremlin
Matangazo ya kibiashara

Mkutano kati ya rais wa Urusi, Vladimir Putin na mwenziye wa Ukraine Petro Porochenko katika mji wa Minsk haukuzaa matunda yoyote. Kwa mujibu wa wizara ya nje ya Marekani, huenda kuingia kwa wanajeshi wa Urusi nchini Ukraine kumepelekea waasi kuwa na nguvu zaidi.

Wayo yakijiri mapigano makali yanaripotiwa katika jimbo la Donetsk tangu Agosti 25, huku serikali ya Kiev ikiendelea kuinyooshea kidole Urusi kwamba wanajeshi wake wamekua wakivuka mpaka na kuingia nchini Ukraine. Urusi kwa upande wake imekua ikikanusha tuhuma hizo dhidi yake. Poland na Jumuiya ya Kujihami ya Mataifa ya Magharibi Nato wamebaini kwamba wanao ushahidi kwamba wanajeshi wa Urusi wamekua wakivuka mpaka na kuingia nchini Ukraine.

Jumatano wiki hii, mwanadiplomasia mmoja wa Nato amethibitisha kwamba kombora linaloweza kushambulia ndege la aina ya SA-22 liliotengenezwa Urusi, limeonekana katika eneo linalodhibitiwa na waasi. Na ushahidi mwingine unaotolewa na Nato ni kombora aina ya SA-11, linalodaiwa kushambulia ndege ya Malaysia Airlines Julai 17, na kusababisha vifo vya watu 298.

Marekani kwa upande wake, imendelea kuilaumu Urusi kwa kuchochea vurugu nchini Ukraine. Balozi wa Marekani nchini Urusi, Geoffrey Pyatt, ameituhumu Urusi kuhusika katika machafuko hayo yanayoendelea mashariki mwa Ukraine.