SYRIA-ALEPPO-MAPIGANO-USALAMA

UN yashindwa kusitisha mapigano Aleppo

Mvulana huyo akipita kwenye vifusi vya mabaki ya nyumba katika kata moja ya mji wa Aleppo, Februari 26 mwaka 2015.
Mvulana huyo akipita kwenye vifusi vya mabaki ya nyumba katika kata moja ya mji wa Aleppo, Februari 26 mwaka 2015. REUTERS/Rami Zayat

Ni pigo kubwa kwa ujumbe wa Staffan de Mistura, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Syria.

Matangazo ya kibiashara

Baada ya majuma kadhaa ya mazungumzo na licha ya juhudi ziyofanywa ikiwa kwa upande wa utawala au kwa upande wa waasi, mchakato wa usitishwaji mapigano ulioanzishwa na Umoja wa Mataifa kwa mji wa Aleppo, umefutiliwa mbali na upinzani wa Syria.

Upinzani umedai mkataba wa jumla kwa taifa nzima la Syria, wala sio kwa mji wa Aleppo peke yake.

 

Kwa mujibu wa mwandishi wa RFI, mjini Beyrut, Paul Khalifeh, katika mkutano uliofanyika katika mji wa Kilis, nchini Uturuki, ambapo alihudhuria kiongozi wa upinzani, ambaye yuko ukimbizini, Khaled Hoja, viongozi wa kisiasa na kijeshi wanaopinga utawala wa Bashar Al Assad mjini Aleppo, wamefutilia mbali mchakato wa msuluhishi wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Staffan de Mistura , unaolenga kusitisha mapigano katika mji huo wa pili nchini Syria.

Upinzani wa Syria haukusubiri kuondoka kwa msuluhishi wa Umoja wa Mataifa katika mji wa Damascus kwa kufutilia mbali mpango wa kusitisha mapigano katika mji wa Aleppo.

Katika taarifa iliyotolewa Jumapili machi 1, Halmashauri ya vikosi vya ukombozi wa mji wa Aleppo, vimefutilia mbali rasimu ya usitishwaji wa mapigano katika mji wa Aleppo, iliopendekezwa na Umoja wa Mataifa. Halmashauri hio iliyowakutanisha Jumamosi Februari 28 wapinzani na wanaharakati wa mashirika ya kiraia katika mji wa Aleppo, katika mji wa Kilis, nchini Uturuki, ambapo kiongozi wa upinzani, aliye ukimbizini, Khaled Hoja, alishiriki mkutano huo, wajumbe wote hao walipinga mpango huo.

Februari 17, Staffan de Mistura, alitangaza mbele ya wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba serikali ya Syria ilikubali kusitisha mashambulizi ya angani katika mji wa Aleppo kwa kipindi cha majuma sita.

Mwishoni mwa juma hili, serikali ilikutana katika mji wa Damascus ili kuhitimisha mpango huo, ambao inaamini kuwa utatekelezwa hata katika mikoa mingine, iwapo utafanikiwa katika mji wa Aleppo.