IRAQ-IS-MAPIGANO-USALAMA

Jeshi la Iraq laingia Tikrit

kifaru cha jeshi la Iraq katika kijiji cha Al Alam, Machi 10 mwaka 2015.
kifaru cha jeshi la Iraq katika kijiji cha Al Alam, Machi 10 mwaka 2015. REUTERS/Thaier Al-Sudani

Baada ya siku kumi ya mapigano makali, na baada ya kukiteka kijiji cha Al Alam, kaskazini mwa Tikrit Jumanne wiki hii, jeshi la Iraq na wanamgambo wa Kishia wamefaulu kwa mara ya kwanza kuingia katika mji wa Tikrit, ngome kuu ya zamani ya Saddam Hussein,

Matangazo ya kibiashara

Mji wa Tikrit umekua ukishikiliwa na kundi la wapiganaji wa Dola la Kiislamu.

Lengo kuu la jeshi la Iraq na wanamgambo wa Kishia ni kuwatimua wanamgambo wa kundi la wapiganaji wa Dola la Kiislamu katika mji huo.

Jeshi la Iraq likishirikiana na wanamgambo wa kishia limeanzisha mashambulizi likilenga kuyadhibiti maeneo muhimu kwa lengo la kuuteka mji wa Tikrit.

Jeshi hilo la Iraq limepata ushindi kusini mwa nchi, baada ya juma lililopita kuuteka mji wa Al Dour, na hatimaye kaskazini baada ya kukiteka kijiji cha Al Alam.

Maeneo hayo mawili ambayo ni ngome mbili kuu muhimu, ilikua ikichukuliwa kama maeneo yatakayopelekea jeshi la Iraq na washirika wake kuuteka kwa urahisi mji wa Tikrit.

Kwa sasa njia imepatikana kwa jeshi la Iraq ya kuingia moja kwa moja Tikrit kwa lengo moja kuu la kuwatimua wanamgambo wa kundi la wapiganaji wa Dola la Kiislamu.

Hata hivyo wanamgambo wa kundi la wapiganaji wa Dola la Kiislamu, wameanza kujielekeza kwa wingi katika mji wa Tikrit ili kuongeza nguvu kwa kikosi cha kundi hilo kinachojiandaa kupambana na jeshi la Iraq.